
Geita. Meya mteule wa Manispaa ya Geita, Leonard Bugomola ameahidi kusimamia ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaomilikiwa na manispaa hiyo, baada ya mradi huo kusuasua kwa zaidi ya miaka mitano.
Bugomola amesema katika awamu hii, watakwenda kuifuta hadithi mbaya ya muda mrefu ya kutokukamilika kwa uwanja huo huku akiamini kuwa utakuwa sehemu ya kuwainua vijana kimaisha kupitia vipaji vyao.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Desemba 02, 2025 wakati akijibu swali la diwani wa kata ya Kanyala, Enock Mapande, aliyehoji kuhusu Meya huyo atakavyolipa kipaumbele suala la mradi huo wa muda mrefu.
‘’Ni kweli mradi wa uwanja umekwama kwa muda mrefu lakini sasa tunakwenda kufuta hadithi ya kutokamilika kwa uwanja na vijana wetu wapate eneo la kuchezea,” amesema Bugomola.
Ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaomilikiwa na Manispaa ya Geita, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh2.4 bilioni ambapo Meya huyo, amewataka wakuu wa idara na watendaji serikalini kuketi na vijana na kusikiliza kero zinazowakabili kwa ajili ya utatuzi badala ya kusubili ujio wa Viongozi wa kitaifa.
‘’Niwaombe watendaji na wakuu wa taasisi,make na viajana muwasikilize madai yao, tusisubili mpaka Waziri wa vijana aje ndiyo wasikilizwe kwa hiyo hili likaandaliwe utaratibu na kutekelezwa kwa haraka,” amesema Mstahiki Meya Bugomola.
Katika taarifa ya robo mwaka wa fedha 2025/2026 iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefredi Myenzi, ameitaja sababu ya kusuasua kwa ujenzi wa uwanja huo kuwa ni mabadiliko ya kanuni za uwekezaji zinazomtaka mwekezaji kusimamia mwenyewe miradi ya kijamii anayoitekeleza. Myenzi amesema kuwa,mradi huo unaotekelezwa kwa thamani ya zaidi ya Sh2.4 bilioni unatarajiwa kuanza baada ya mradi huo kukabidhiwa katika kampuni ya uchimbaji madini Geita Gold Mine Limited (GGML).
‘’Mradi ulisimama mwaka 2023 na mkandarasi aliyekuwepo kusitishiwa mkataba ambapo mabadiliko ya kikanuni yanamtaka mwekezaji kusimamia miradi ya kijamii (CSR) mwenyewe hivyo kwa sasa GGML walichukua mradi huo na ndiyo wanaousimamia na kuujenga kwa hiyo tunasubili wakamilishe taratibu za kumweka mkandarasi atakayeujenga mpaka mwisho,’’ amesema Myenzi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita,Barnabas Mapunda,amewataka madiwani kuweka kipaumbele katika ujenzi wa uwanja ikiwa ni pamoja na kuisaidia timu ya Geita Gold FC kurejea ligi kuu na hatimaye kimataifa kwa kuwa mkoa huo una wafadhili wanaoweza kuiinua timu hiyo.
‘’Tuwasaidie vijana wawe na mahali pa kuchezea, yamkini miundombinu ingekuwa mizuri wasingekwenda hata kufuata mkumbo wa mambo yasiyofaa katika jamii, niwaombe sana madiwani, kuna kipindi tulifika hadi kimataifa lakini sasa tunashindwaje? Tuwasaidie vijan kupitia michezo,” amesema Mapunda.
Kikao hicho kilikuwa cha kwanza kwa baraza jipya la madiwani ambapo madiwani wamemchagua kwa Leonard Bugomola kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Geita kwa kura zote 20 za wapigakura huku Elias Ngole akichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo.