Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya Umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imetwaa ubingwa wa mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa umri huo (AFCON U17) baada ya kuichapa Uganda kwa mabao 3-2 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mashindano hayo yako chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa ajili ya kutafuta timu tatu za kuwakilisha Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika Fainali za AFCON U17, mwakani huko Morocco.
Katika mchezo wa leo Serengeti Boys ilipata mabao yake kupitia kwa Razack Juma aliyefunga mawili na Luqman Mbalasalu aliyepachika moja.
Ushindi huo umeifanya Serengeti Boys kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa fainali wa mashindano hayo mwaka jana mbele ya Uganda ambayo ilifungwa mabao 2-1.
Lakini pia huo ni ubingwa wa kwanza ambao Serengeti Boys imetwaa wa mashindano hayo kwani tangu yalipoanza rasmi 2018, haikuwahi kutwaa taji.
Timu zote mbili Tanzania na Uganda pamoja na mshindi wa tatu, Ethiopia zimefanikiwa kufuzu Fainali za AFCON U17, zitakazofanyika Morocco mwakani.
Fainali hizo za AFCON U17, zitashirikisha idadi ya timu 16 zitakazogawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja.
Fainali hizo za AFCON U17 zitatoa pia timu 10 zitakazoshiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri mwaka 2027.