Katika ujumbe wake mahsusi kwa siku hii Katibu Mkuu Guterres anasema “watu wenye ulemavu si washiriki pekee bali ni wanamageuzi katika jamii.”

Ameonya kuwa watu wenye ulemavu bado mara nyingi wanatengwa kwenye meza za maamuzi yanayohusu maisha yao.
Amesistiza kuwa “Watu wenye ulemavu wanaongoza ubunifu, wanaathiri sera, na wanahamasisha haki. Hata hivyo mara nyingi wananyimwa nafasi katika kufanya maamuzi.”

Kauli mbiu ya siku ya mwaka huu ni “Kukuza jamii jumuishi kwa watu wenye ulemavu kwa kusongesha maendeleo ya kijamii”  kaulimbiu hii inaendeleza  moja kwa moja na mwamko wa Mkutano wa Pili wa Dunia wa Maendeleo ya Kijamii uliofanyika Doha Qatar mwezi uliopita. Mkutano huo ulipitisha Tamko la Kisiasa la Doha, ambalo Guterres anasema limetoa ujumbe ulio wazi, “Hakuna maendeleo endelevu bila ujumuishaji wa watu wenye ulemavu.”

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza mchango muhimu wa watu wenye ulemavu katika kusukuma maendeleo duniani ukijumuisha kuboresha maandalizi ya kukabili majanga, kupanua wigo wa elimu shirikishi na ajira,
na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia walio hatarini zaidi.

Mkuu huyo wa Umoja wa Maataifa ameikumbusha dunia kwamba baadhi ya ubunifu tunaotumia kila siku ulianzishwa na kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Alkitolea mfano “Ujumbe mfupi wa maandishi, teknolojia ya sauti kuamsha kifaa  vyote vilianza kama suluhisho lililobuniwa na watu wenye ulemavu.”

Lakini amesisitiza kuwa changamoto za muda mrefu bado zipo. Ubaguzi, umaskini, na huduma zisizofikika bado zinawazuia zaidi ya watu bilioni moja duniani kote.

Guterres ametoa wito wa kuchukua hatua madhubuti na ushirikiano wa kweli akisistiza kwamba “Katika Siku hii ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu, tujitahidi kufanya kazi bega kwa bega na watu wenye ulemavu, katika utofauti wao wote, kama washirika sawa.”

Amehitimisha ujumbe wake kwa kukumbusha kwamba ujumuishaji unapotekelezwa kikamilifu, faida ni kwa wote na kuongeza kuwa “Ujumuishaji unapokuwa halisi, kila mtu hunufaika. Pamoja, tunaweza kujenga jamii zinazofikika zaidi, zenye mnepo, ambamo sote tunastawi.”
Umoja wa Mataifa unasema maadhimisho ya leo si tu kumbukizi, bali ni wito mpya wa kuchukua hatua kwa usawa, upatikanaji wa huduma, na utambuzi kwamba jamii jumuishi ni jamii imara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *