Onyo hilo limetolewa leo  katika mkutano wa waandishi wa habari unaofanyika Geneva, ambapo wakuu wa UNMAS wamewasilisha taarifa za uwanjani zinazoonesha kuongezeka kwa uchafuzi wa vilipuzi, idadi ya vifo na majeruhi hasa miongoni mwa raia pamoja na changamoto kubwa zinazoikabili operesheni za kibinadamu. Ongezeko la vilipuzi na vikwazo vya upatikanaji wa maeneo ya walioathirika limeelezwa kuwa sababu kuu ya tahadhari hiyo.

Afghanistan: Watoto wanawakilisha asilimia 80 ya waathiriwa wote

“Afghanistan inabaki kuwa moja ya maeneo hatari zaidi duniani kwa vilipuzi,” amesema Nick Pond, Mkuu wa Uondoaji Mabomu wa UNAMA.
Nick Pond ameeleza kuwa, Afghanistan ina idadi ya tatu kwa juu duniani ya waathiriwa wa vilipuzi mwaka 2024, zaidi ya watu 54 kwa mwezi wanauawa au kujeruhiwa, na asilimia 80 ni watoto.
Amebainisha kuwa wengi wa waathiriwa ni wavulana wanaochunga mifugo vijijini.

Ni watoto, hasa wavulana wanaochunga kondoo na mbuzi milimani, wanachukua vitu vinavyowavutia, wanacheza navyo, au kuvipigia mawe na kujeruhi au kuuawa. Licha ya kiwango kikubwa cha uchafuzi, uwezo wa uondoaji mabomu umeporomoka kwa kiasi kikubwa. Mwaka 2011 kulikuwa na wafanyakazi 15,000 wa kuondoa mabomu, na sasa tumebakiwa na takriban 1,300,” amesisitiza

Sudan: Uzingirwa wa El Fasher na taarifa za mabomu yatia wasiwasi

Sediq Rashid, Mkuu wa UNMAS Sudan amesema mgogoro nchini Sudan, hususan El Fasher, umeongeza hatari kubwa kwa raia na wafanyakazi wa misaada. 
Pia amesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu hali huko El Fasher, kwa sababu imezingirwa kwa zaidi ya siku 500 na mashambulizi hayajakoma,na kuna taarifa za uwepo wa mabomu ardhini.

Rashid ameonya kuwa upatikanaji bado ni mdogo sana na kuwa Kordofan inajitokeza kama kitovu kipya cha hatari.
Ameongeza kuwa timu zote tano za uondoaji mabomu ziko Khartoum zikijibu tu vitisho vya dharura.

Hawafanyi usafishaji wa kimfumo wanajibu vipaumbele vya dharura pekee,” amesema.

Gaza: Uchafuzi ‘mkubwa kupindukia’ baada ya miaka miwili ya mapigano

Katika Ardhi ya Palestina inayokaliwa kimabavu, UNMAS imeeleza kiwango kikubwa sana cha uchafuzi wa vilipuzi baada ya mapigano ya muda mrefu.

Baada ya miaka miwili ya mapigano makali, kiwango cha uchafuzi wa vilipuzi Gaza ni kikubwa kupindukia,” amesema Julius Van Der Walt, Mkuu wa UNMAS Gaza.

Amesema uchafuzi huo unazuia moja kwa moja shughuli za kibinadamu na juhudi za kurejesha huduma.
Amesisitiza kuwa uchafuzi unatishia jamii moja kwa moja na unazuia msaada muhimu kwa wakaazi milioni 2.1, unachelewesha mipango ya ukarabati wa awali na kufanya ujenzi upya kuwa hatari sana.

Nigeria: Raia hatarini kufuatia kufungwa kwa kambi za wakimbizi wa ndani

Nchini Nigeria, sera za kuwarejesha watu makwao zimewaweka raia katika hatari, walianza kufunga kambi za wakimbizi wa ndani na kuwahimiza watu kurudi, lakini uchambuzi wetu unaonesha asilimia 80 ya waathiriwa wa raia wako katika maeneo 11 kati ya 15 ya kurejea,” amesema Edwin Faigmane, Mkuu wa UNMAS Nigeria.

Ili kupunguza hatari, UNMAS inafanya kazi na vikosi vya usalama kutoa elimu ya hatari na kuboresha mifumo ya taarifa.
Tumeanza kufanya kazi na vikosi vya usalama kupeleka elimu ya hatari katika maeneo magumu kufikiwa. Hilo limeleta matokeo, kwani sasa wanajamii wanaripoti vitu vinavyoshukiwa kuwa vilipuzi ” amefafanua.

Wito wa kuongeza rasilimali na kuboresha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu

Katika maeneo yote manne, maafisa wa UNMAS wameonya kwamba kuongezeka kwa uchafuzi huku upatikanaji ukipungua na ufadhili usiotosha kunaweza kuzidisha migogoro ya kibinadamu.
Wametaka jamii ya kimataifa kuongeza msaada ili kulinda raia, kuwezesha utoaji wa misaada kwa usalama, na kujenga upya uwezo wa uondoaji mabomu katika baadhi ya maeneo hatari zaidi duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *