Je, unajua msichana 1 kati ya 6 wenye umri wa miaka 15-19 nchini Kenya anapata mimba au tayari ni mama, na hivyo kusababisha zaidi ya mimba 260,000 kila mwaka? Hii ni simuliziya mmoja wa vijana nchini Kenya ambaye ameamua kukumbatia msaada wa UNFPA na kusaka hudumaza afya ya uzazi ili aweze kutimiza ndoto zake. 

“Jina langu ni Lucy Achieng Odhiambo, nina umri wa miaka 18. Nilimaliza elimu ya sekondari mwaka jana 2024 na nilikuwa katika shule ya bweni. Niliporudi nymbani nikagundua kwamba wasichana wengi wako na changamoto nyingi sana,  wengine wamepata au wanaweza kupata mimba za utotoni.”

Wasichana vigori wanakabiliwa na vikwazo  vya kupata huduma za afya ya uzazi na matibabu ya virusi vya UKIMWI, VVU au njia za kujikinga dhidi ya virusi hivi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa taarifa kuhusu huduma hizi, ukosefu wa kifedha, safari ndefu ya kusaka huduma za afya, na shinikizo la kijamii na kitamaduni. Mapengo haya huwaacha wengi bila kuhudumiwa, au kuwa na nyenzo za kutosha kulinda afya zao.

Lucy anasema kuchukua hatua ya mpango wa uzazi kama msichana haimanishi wewe unajihusisha na vitendo vya ngono kiholelaholela..

“Kutumia njia ya uzazi wa mpangohaimaanishi wewe ni yule wa kufanya ngono kila mara, la hasha.Mimi nimekumbatia huduma hizi na kutumia mpango wa uzazi kwa sababu niko na ndoto yangu, ninataka kuendelea na masomo na kumaliza shule halafu baada ya haponikishapata kazi niwe na kids badala ya sasa hivi.”

Umoja wa Mataifa umeendelea kusimama na vijana hao vigori na kuhakikisha wamepata nafasi bora ya kushauriana na wahudumu wa afya, na kuweza kupanga mustakabali wao. Dkt. Stephen Jackson, Mratibu Mkazi wa Umoja huo mjini Nairobi Kenya anasema

”Wasichana ambao hawapati mimba katika ujana wao wana nafasi nzuri zaidi za kumaliza shule, kupata matokeo bora ya elimu, matokeo bora ya kiafya, ambayo yanaboresha usawa wa kijinsia, na kwa ujumla hilo bila shaka husaidia kujenga jamii yenye nguvu na thabiti zaidi katika taifa la Kenya, kuimarisha uchumi wa Kenya na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu nchini Kenya.”

Kupitia mpango huu wa UNFPA, sasa Lucy Achieng na vijana wenzake wanapata msaada wanaohitaji. Lucy anaweza kuuliza maswahi na apate taarifa sahihi,  na anaweza kuwa na chaguo linalofaa kwa maisha yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *