Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan vilivyodumu mwaka wa tatu sasa vimewalazimisha mamilioni ya watu kufungasha virago na kuyahama makazi yao, vikitsambaratisha jamii nzima. Li Fung, Mwakilishi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mstaifa nchini humo anasema ukubwa wa janga hili hauwezi tena kupuuzwa.
“Hali hii kwanza kabisa ni mgogoro wa haki za binadamu. Kiwango cha ukatili wa ukiukaji tunaoendelea kurekodi vinaonesha janga ambao limesambaratisha maisha ya mamilioni ya watu na kuwapokonya Wasudan haki ya ulinzi ambao kila binadamu anastahili”
(Katikati) Li Fung, Mwakilishi wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu (OHCHR) nchini Sudan, alipotembelea Bandari ya Sudan akiwa na Radhouane Nouicer (kulia), Mtaalam Mteule wa Sudan wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.
Wachunguzi wa haki za binadamu wanaendelea kugundua ukatili mpya kila uchao. Fung anaonya kuwa ghasia hizo sasa zinachukua mkondo hatari unaochochewa na mrengo wa kikabila, huku taasisi za sheria na haki zikifungwa mdomo kutokana na kudhoofika kwa kiasi kikubwa
“Tunarekodi mauaji ya kiholela, ukatili wa kingono, utekaji na watu kutoweshwa kwa lazima. Tunatiwa wasiwasi mkubwa na kuongezeka kwa vurugu na chuki za kikabila.”
Kwa kupwaya kwa taasisi muhimu za ulinzi wa raia, Fung anasema juhudi za kuleta uwajibikaji sasa zinategemea hatua za kimataifa kuanzia ufadhili wa kibinadamu hadi shinikizo la kisiasa kusitisha mtiririko wa silaha na kuzirejesha pande zinazopigana kwenye meza ya mazungumzo.
Hata hivyo, pamoja na hali kuwa mbaya, Fung anasema raia wa Sudan wanaendelea kuonesha ujasiri wa hali ya juu, wakisaidiana katika mazingira magumu zaidi.
Mtoto wa Sudan katika KAMBI ya DALI, TAWILA – Darfur. Familia yake ilikimbia El Fasher, ambapo njaa iliyokuwa ikiendelea ilithibitishwa mnamo Oktoba 2025
Kuelekea Siku ya Haki za Binadamu, Fung anasema ujumbe wako uko bayana kwa pande zote zinazopigana nchini Sudan.
“Haki za binadamu za watu wa Sudan lazima zilindwe. Pande zote lazima ziheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. Watu wa Sudan wanastahili amani, haki na kuheshimiwa kwa haki zao za msingi.”
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa bila hatua za dharura za kimataifa sasa, Sudan inaweza kuzama zaidi katika janga kubwa la kibinadamu lisiloelezeka.