Serikali ya Tanzania imewaonya raia wake kutothobutu kuingia mitaani, ikisema maandamano yoyote ya Desemba 9 ni kinyume na sheria na yatachukuliwa kama jaribio la mapinduzi.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kusalia majumbani mnamo Desemba 9, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Uhuru wa Tanganyika. Kauli hiyo ilitolewa siku ya Jumatatu Desemba 8 na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kufuatia kuibuka kwa taarifa za wito wa maandamano unaosambaa kupitia mitandao ya kijamii, hatua iliyoifanya serikali kuongeza tahadhari kuelekea siku hiyo muhimu ya kitaifa.

Ulinzi umeimarishwa sehemu mbalimbali hasa katika miji mikubwa kwa kuenezwa vikosi vya polisi na wanajeshi waliojihami kwa silaha. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuondolewa kwa marufuku hiyo  na kuvitaka vyombo vya usalama kutotumia nguvu kupita kiasi katika kudhibiti maandamano hayo.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa kishindo wa uchaguzi wa Oktoba baada ya wapinzani wake wakuu kutengwa, na kusababisha maandamano ambayo kwa kiasi fulani yalichochewa na kile wanaharakati walisema ni ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani.

Makundi ya haki za binadamu, vyama vya upinzani na Umoja wa Mataifa vimesema mamia ya watu huenda waliuawa katika makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama. Serikali inakanusha kukandamiza upinzani na inapinga takwimu hizo ikitaja kuwa ziliozidishwa.

Msemaji wa Polisi David Misime alisema bado hawajapokea arifa zozote rasmi kutoka kwa mtu yeyote anayetaka kufanya maandamano, baada ya machapisho ya mitandao ya kijamii kusambaa ya kutaka maandamano yafanyike Desemba 9.

“Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano haya, ambayo yamepewa jina la ‘maandamano ya amani yasiyo na kikomo,” David Misime alisema siku ya Ijumaa katika taarifa.

Misime alisema wale walioandaa maandamano, miongoni mwa mambo mengine, walikuwa wakiwahimiza washiriki kukamata mali, kuvuruga huduma hospitalini na kukaa mitaani kwa muda usio na kikomo ili kudhoofisha shughuli za kiuchumi.

Siku ya Jumatano, kundi la wataalamu wa haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilizitaka mamlaka za Tanzania na vikosi vya usalama kulinda haki ya watu ya kukusanyika na kuzuia ukiukwaji wowote zaidi kabla ya maandamano yaliyopangwa.

Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuchunguza vurugu za uchaguzi na kutoa rambirambi kwa familia zilizofiwa, jambo ambalo limemfanya akubali waziwazi machafuko hayo, ambayo yamesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa nchini kwa miongo kadhaa.

“Tunasikia kuna maandamano mengine yaliyopangwa … kila wanapokuja, tuko tayari,” Hassan aliambia mkutano wa wazee jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne wiki iliyopita, akimaanisha maandamano yaliyopangwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *