
Serikali ya Marekani imezidisha mashinikizo kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ili kukubali kuachia sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo na makubaliano mengine yaliyoainishwa katika mpango wa amani wa mwenzake wa Marekani Donald Trump.
Maafisa wawili wa Ukraine ambao majina yao hayawekwa wazi wamenukuliwa na tovuti ya habari ya Axios wakisema kuwa Zelensky anakabiliwa na “mashinikizo makubwa ya Washington” baada ya mkutano wa hivi majuzi kati ya washauri wa Trump na Rais Vladimir Putin wa Russia kuhusu mpango wa amani, ambao kwa mujibu wake, Ukraine italiachia eneo lote la Donbas mkabala wa Marekani kuipatia dhamana kubwa ya usalama itakayozuia operesheni za kijeshi za Russia dhidi ya nchi hiyo.
Afisa mmoja wa Ukraine amenukuliwa na toviti ya Axios akisema kuwa: ” Chaguo la Marekani ni baya sana kwa Kiev baada ya washauri wa Trump yaani Steve Witkoff na Jared Kushner kukukutana na kuzungumza kwa masaa matano na Rais Putin wiki iliyopita huko Kremlin.
Afisa huyo amebainisha kuwa: Witkoff na Kushner walionekana kutaka kupatiwa jibu la wazi la “ndiyo” kutoka kwa Zelensky walipojadiliana naye mpango huo katika mazungumzo ya simu yaliyodumu kwa masaa mawili siku ya Jumamosi.
Afisa mwingine wa Ukraine pia amesema, pendekezo la Marekani limejumuisha masharti magumu zaidi kuliko matoleo ya awali kuhusu masuala kama vile udhibiti wa kinu cha nyuklia huko Zaporizhzhia, na limeacha maswali muhimu kuhusu dhamana ya usalama bila kujibiwa .
Amesema, kuna kadhia muhimu na kubwa kuhusu udhibiti wa maeneo yanayohitaji kujadiliwa pakubwa; yaani nani abaki wapi, na upande upi unajiondoa. Na iwapo Ukraine itajiondoa kwenye laini ya mawasiliano, ni kwa naman ipi Ukraine itahakikishiwa kuwa Russia inafanya vivyo hivyo na haiendelei na mapigano dhidi ya Kiev.”