
Kibaha. Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani imeingia katika hatua za mwisho za maandalizi makubwa ya kuwapokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza mwaka 2026, ambapo zaidi ya wanafunzi 6,000 wanatarajiwa kuanza masomo yao mwezi Januari.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeanza shule akiwa hana dawati na katika kutekelza hilo zaidi ya sh. 400 milioni zikitengwa kwa ajili ya utengenezaji wa madawati.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 10, 2025 na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Nicas Mawazo, amesema maandalizi hayo yamepiga hatua kubwa na yanatarajiwa kukamilika muda mfupi kabla ya shule kufunguliwa.
“Tumehakikisha kila mwanafunzi atakayepangiwa kuanza kidato cha kwanza anakuwa na dawati lake. Hatuwezi kuruhusu mtoto aanze masomo akiwa anakaa chini, amesema Dk. Mawazo.
Kwa mujibu wa taarifa za Idara ya Elimu ya Manispaa hiyo, idadi ya wanafunzi wa mwaka huu imeongezeka kutoka wanafunzi 4,800 mwaka jana hadi 6,000 mwaka huu, ongezeko linaloonyesha uhitaji mkubwa wa miundombinu ya elimu katika mji huo unaokua kwa kasi.
Baadhi ya wakazi wa Kibaha wamepongeza hatua hizo, wakisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kuboresha mazingira ya elimu ili wanafunzi wasome kwa utulivu.
Faidha Mussa, mkazi wa Maili Moja, amesema ni muhimu madawati hayo kufika kwa wakati ili wanafunzi wote wanufaike.
Amesema watoto wanapokaa chini wanakosa umakini darasani na kusisitiza utekelezaji uwe wa haraka.
Amani John amesema mazingira bora ya kujifunzia yana mchango mkubwa katika kuongeza ufaulu.
Alisema wanafunzi wanahitaji kujisikia salama na starehe darasani, na kwamba madawati ni sehemu ya msingi wa elimu bora.
Kwa upande wake, Halima Noah amesisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa karibu ili madawati yasibaki kwenye maghala.
Amesema ni vizuri kuona yanatengenezwa, lakini muhimu ni kuhakikisha yanawafikia shule zote kwa wakati.
Hadi sasa, zaidi ya asilimia 85 ya kazi za utengenezaji wa madawati na ukarabati wa madarasa zimekamilika, hatua inayotarajiwa kuwezesha wanafunzi wote wapya kuanza masomo bila changamoto yoyote Januari mwaka 2026.