Dar es Salaam. Kati ya wasanii wa hip hop Bongo wanaoendana na soko la sasa Young Lunya ni miongoni mwao kwa sababu ngoma zake zimekuwa zikipata mwitikio mkubwa kutoka kwa vijana wengi hasa wa rika la kati.

Akiwa ametoa albamu na kushinda tuzo, muziki wake unagonga namba kubwa katika majukwaa ya mtandaoni huku akiendelea kushirikiana na wasanii wa ndani na hata kimataifa. Fahamu zaidi.

1. Young Lunya alifanya muziki katika kituo cha Mkubwa na Wanawe kilichowatoa wakali kibao Bongo kama Aslay na Mbosso, ila baada ya muda akaendelea na harakati zake nyingine hadi alipokuja kutoka.

LUNY 01

2. Alipata usikivu wa wengi akiwa kundi la OMG ambalo alikuwa na wenzake wawili, Salmin Swaggz na Conboi. Walivuma zaidi na ngoma yao, Uongo na Umbea (2017) wakiwa na Barakah The Prince. Kundi hilo lililofanya zaidi miondoko ya trap, wote walisainiwa na Switch Music Group (SMG), rekodi lebo yake rapa Quick Rocka.

3. Ni Quick Rocka aliyempa Young Lunya jina la OMG baada kuona ana uwezo mkubwa katika kuchana ila rapa huyo hakuwa tayari kulitumia ndipo likageuka kuwa la kundi lao. Utakumbuka Quick Rocka ambaye aliunda kundi la Rockaz na wenzake watatu Chief  Rocka, Dau Rocka na Mo Rocka, nao walipewa jina hilo (Rockaz), na hayati Ngwair kufuatia kuridhika na uwezo wao. 

LUNY 02

4. Hapo awali Young Lunya alikuwa anapenda kucheza mpira wa kikapu, sasa huko kwenye kikapu ndipo akakutana na watu wa Hip Hop na kuvutiwa na aina hiyo ya muziki.

5. Kufanya vizuri kwa wimbo wake, Mbuzi (2021) kulimuwezesha kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2021 – akishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop. Hivyo albamu yake ya kwanza iliyokuja kutoka Juni 2024, akaamua kuipa jina la ‘Mbuzi’ ikiwa na nyimbo 11 na kushirikisha wasanii 10 kutoka nchi nne tofauti. 

6. Kati wasanii wa waliosikika katika albamu hiyo ni pamoja na Mr. II Sugu ambaye ni mshindi wa TMA 2000 kama Msanii Bora wa Hip Hop, huku akiwa ametoa albamu 10.

7. Kolabo yake na Khaligraph Jones kutokea Kenya, Stupid (2023), ilishinda tuzo ya TMA 2023 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop. Hivyo Lunya kupitia ngoma zake mbili (Mbuzi na Stupid), ameshinda tuzo nne za TMA akiwa rapa pekee aliyeshinda mara nyingi zaidi tangu kurejea tuzo mwaka 2022 baada ya kusimama kwa miaka saba.

LUNY 03

8. Seven Mosha alishawishika na uwezo wa Young Lunya baada ya kuchana katika mdundo wa wimbo wa Ommy Dimpoz, Kata (2020), ndipo akaona anafaa kusainiwa Sony Music. Ikumbukwe Seven ndiye Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, nafasi anayoitumikia tangu Desemba 2020.

9. Seven alipenda jinsi Young Lunya anajua kuchugua maneno ya kuyatumia katika rap, midondoko yake na uwasilishaji wa kuvutia ambao unabeba uhusika fulani wa kuaminisha kitu kinachozungumziwa.

10. Na kabla hata Seven hajapendekeza Young Lunya kusainiwa Sony Music, tayari alishasikiliza albamu ya rapa huyo ambayo bado ilikuwa haijatoka na kuona ni mwanamuziki mwenye uwezo na kiu ya kufika mbali. Ni Seven Mosha ambaye ana uzoefu wa miaka zaidi ya 20 katika tasnia akihusika katika miradi kadhaa mikubwa ya kimataifa nchini kama Coca Cola Popstar (2004), Jay Z Water for Life Tour (2006), One8 (2010) na kadhalika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *