Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na utaratibu mpya katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva kila msanii anayesainiwa na kutambulishwa kwenye lebo za Bongo basi lazima aachie wimbo unaohusu kuumizwa.
Iwe ni hadithi ya kuachwa, kupuuzwa, kusalitiwa au kuumizwa na mapenzi mziki wa majonzi umekuwa kama mlango wa kutambulisha wasanii wapya.
Cha kushangaza ni, nyimbo hizi siyo tu zimekuwa zikivutia mashabiki, bali pia zimekuwa zikifanya vizuri zaidi kwenye mitandao ya kijamii, redio na chati za muziki kuliko nyimbo za midundo ya furaha.
Inaonekana kuwa hisia za maumivu ni lugha ya pamoja inayowaunganisha wasikilizaji na hivyo kumrahisishia msanii mpya jambo ambalo limekuwa kama desturi kwa wasanii wengine wanaotambulishwa.
Mwananchi limekuchambulia baadhi ya wasanii waliotambulishwa kwenye lebo wakaachia albamu au Extended Playlist wakaanza na nyimbo za kuumizwa.
1. Dvoice (Umenifunza)
Ana miaka miwili sasa tangu atambulishwe rasmi Lebo ya Wasafi Novemba 17,2023 akiwa msanii wa saba baada ya Harmonize, Rich Mavoko, Rayvanny, Mbosso, Zuchu na Lavalava.
Baada ya kutambulishwa siku hiyo Dvoice aliachia albamu ya Swahili Kid yenye ngoma 10, akiwashirikisha wasanii wengine wa Wasafi akiwemo Zuchu (Bambam na Nimezama), Diamond Platnumz (Kama wengine) Mbosso (Mpeni taarifa) na Lavalava (Turudiane) kabla ya kutoka kwenye lebo hiyo.
Kiufupi Swahili Kid ni albamu inayojumuisha mchanganyiko wa mitindo ya muziki kama Singeli, Bongo Fleva, Amapiano, Afro Pop na Zouk, huku ikigusa pia maudhui ya kijamii, mapenzi, maumivu, ugumu wa maisha na mengine mengi.
Katika albamu hiyo Umenifunza ni wimbo uliokuwa unahusu maisha ya vijana na changamoto wanazokutana nazo katika mahusiano yao. Pia unazungumzia namna umaskini unavyoweza kusababisha mtu kuhisi aibu, udhalilishaji au kujiona hana thamani.
Ikumbukwe Dvoice kabla hajasainiwa Wasafi alikuwa akitambulika kama msanii wa singeli lakini alipotambulishwa na kuzindua ngoma ya kwanza yenye ya Bongo Fleva.
2. Zuchu (Nisamehe)
Alipotambulishwa mwaka 2020 aliachia Extended Playlist (EP) yake, I Am Zuchu iliyokuwa na nyimbo 13 ikiwemo Wana, Kwaru, Raha, Ashua na Mbosso na Mauzauza akimshirikisha mama yake mzazi gwiji wa muziki wa Taarab, Khadija Kopa.
Lakini katika ngoma hizo zenye mchanganyiko wa Taarab, Bongo Fleva na mapenzi lakini kibao cha Nisamehe kilikuwa cha tofauti kilichogusa hisia za mashabiki zake akiyaimba na kuyalilia mapenzi.
Katika listi ya ngoma zake Nisamehe ilifanya vizuri zaidi ikiwa na watazamaji zaidi ya Milioni 24 kwenye mtandao wa Youtube.
3. Mac Voice (Nenda)
Wakati anasainiwa Next Level Music chini ya Rayvanny aliachia EP yenye ngoma tano kati ya hizo mbili zilikuwa zinahusu kuumizwa kwenye mapenzi.
Ngoma hizo ziliachiwa mwaka 2021 Nenda na Bora Peke Yangu akimshirikisha bosi wake wa zamani Rayvanny kabla hajatimka kwenye lebo hiyo mwaka 2024 yaani alihudumu miaka mitatu tu.
Nyimbo hizo zilifanya vizuri hasa Nenda ambayo ilikuwa inaeleza kwa kina namna alivyompenda mtu lakini kumbe naye anampenda mwingine na baada ya muda anaondoka.
Licha ya Mac Voice kwa sasa kutovuma kama ilivyokuwa miaka mitatu alipokuwa Next Level, lakini hadi sasa Nenda inaendelea kusikilizwa na kufanya vizuri ikiwa na zaidi ya watazamaji Milioni 17 Youtube.
4. Yammi (Namchukia)
Wakati Yammi anaingia kwenye lebo ya African Prncess chini ya mwanadada Nandy mwaka 2023 naye aliachia EP ya Three Hearts yenye ngoma tatu tu kati ya hizo mbili zilihusu kuumizwa kihisia.
Aliachia mikwaju miwili Hanipendi na Namchukia, lakini Namchukia ilipata umaarufu mkubwa na kuanza kumjengea jina mwanadada huyo aliyeachana na lebo hiyo mapema mwaka huu.
Maudhui ya video hiyo iliyoachiwa miaka miwili iliyopita yanaonesha ujumbe wa maumivu ya moyo yaliyosababishwa na mtu aliyewahi kumpenda.
Kutoka kuwa kwenye penzi la dhati hadi kufikia hatua ya kuchukiwa na mtu aliyewahi kuitwa mchumba wa maisha yake.
Ni ngoma inayohusu hadithi ya safari ya kuumiza, huzuni nzito na jinsi mapenzi yanavyoweza kubadilika ghafla kutoka kwenye upendo hadi chuki kutokana na majeraha ya moyo.
5. Ibraah (Nitachelewa)
Ibraah alitambulishwa Konde Gang mwaka 2020 kwa kushirikishwa na Harmonize kwenye ngoma ya One Night Stand na humo alionyesha umahiri wa kuimba sauti, kucheza na kamera ingawa ilikuwa mara yake ya kwanza.
Baada ya kolabo hiyo ndipo aliachia Nitachelewa ikiwa ngoma yake peke yake, licha ya ugeni kwenye gemu ya Bongo Fleva kibao hicho kilifanya vizuri na kuingiza zaidi ya watazamaji Milioni 14 hadi sasa Youtube.
Katika wimbo huu, Ibraah anatuambia jinsi alivyoumia sana kwa sababu ya mpenzi wake wa dhati.
Anaeleza machungu aliyopitia na jinsi ambavyo haoni kama maumivu hayo yanaweza kupona kirahisi.
Hii ndiyo sababu aliuita wimbo wake Nitachelewa, akimaanisha kuchelewa kwake kupona, kurudi kwenye hisia nzuri za mapenzi, au hata kuamini tena katika mapenzi baada ya kuumizwa.
6. Maua Sama (Namwachia)
Ametengeneza EP mbili Cinema (2022) na Sama (2024) ambazo zote mbili alimshirikisha Ali Kiba Nioneshe na Itakuwaje.
Katika EP ya Cinema aliachia ngoma nane lakini moja ya Namwachia ilikuwa inaeleza ujumbe tofauti wa maumivu kwa mtu aliyempenda.
Ni kama Maua Sama aliingia kwenye mtego wa wasanii wanaotambulishwa basi lazima ngoma ya kuumizwa iwepo na zimekuwa zikifanya vizuri kuliko hata nyingine.
Katika maelezo ya ngoma hiyo ilieleza “Siku niliyorekodi wimbo huu, baada ya kumaliza beti ya mwisho, nililia sana. Niliumia kwa jinsi Yogo alivyoandaa rhythm hii, na zaidi nilipohisi jinsi sauti yangu ilivyokuwa imejaa huruma na malalamiko kuhusu matatizo niliyokuwa napitia wakati huo.”