Hafla hiyo imesisitiza umuhimu wa milima kwa uhai, ikazindua muhtasari wa kiufundi, na kutangaza washindi wa Tuzo ya milima ya Mountain Future 2025.
Takribani asilimia 70 ya maji safi duniani yanapatikana katika theluji na barafu, na maji yatokanayo na kuyeyuka kwa barafu yanawawezesha karibu watu bilioni 2 kupata maji ya matumizi ya kila siku, kuendesha nishati ya maji, kilimo, viwanda na kuhifadhi bioanuwai limesema shirika hilo.
Hata hivyo, FAO inasema barafu zinaendelea kuyeyuka kwa kasi isiyowahi kushuhudiwa, na hivyo kuongeza hatari ya ukosefu wa maji, majanga ya asili na uhaba wa chakula kwa jamii za milimani na maeneo ya chini.
Kaulimbiu ya mwaka huu inaangazia changamoto zinazoendelea na fursa katika maendeleo ya milima, pamoja na kuimarisha ushirikiano unaowezesha matokeo chanya kwa jamii na mazingira ya milimani duniani.
“Jamii za milimani zinaendelea kuonesha ubunifu wa kipekee uliolinda mifumo tete ya ikolojia kwa karne nyingi. Tunahitaji kuongeza msaada kwa jamii hizi ili ziweze kubadilisha changamoto hizo kuwa fursa,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, katika ujumbe wa video kwenye hafla ya ngazi ya juu kusdhimisha siku hii.
Qu amesema kuwa FAO tayari imeunga mkono ujenzi wa barafu bandia nchini Kyrgyzstan, ambazo katika baadhi ya maeneo zimehifadhi zaidi ya mita za ujazo milioni 1.5 za barafu kiasi kinachotosha kumwagilia mashamba.
Ameongeza pia kuwa nchini Bolivia, FAO na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) wanasaidia kufunga vitambuzi kwenye barafu kwa ajili ya kufuatilia theluji na kuyeyuka kwake, ili kuwapa wakulima na watunga sera taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa maji.
Jamii za milimani hususan vijana na watu wa jamii za asili ndizo zinazoathiriwa moja kwa moja na mabadiliko haya, hivyo kuzifanya kuwa wahusika muhimu katika kutafuta suluhu bunifu na juhudi za kuhimili mabadiliko.
Mkoa wa Tibet una sifa ya baadhi ya milima mirefu zaidi duniani.
Uzinduzi wa sera
Muhtasari wa kiufundi uliopewa jina “Barafu na milima, muingiliano wa uhakika wa chakula, maji na riziki” umezinduliwa katika hafla hiyo, ukisisitiza nafasi muhimu ya barafu na maeneo ya theluji katika kuendeleza uzalishaji wa chakula, riziki na usalama wa maji katika milima na maeneo ya chini.
FAO inasema
- Maji yatokanayo na barafu ni uti wa mgongo wa uzalishaji wa chakula, yakinufaisha kilimo kuanzia mashamba ya juu ya milimani hadi mashamba makubwa ya umwagiliaji.
- Kuyeyuka kwa barafu kunavuruga mifumo ya chakula na maisha vijijini kwa kupunguza mavuno, kuhatarisha mifugo na kuongeza hatari kwa jamii.
- Kilimo endelevu na mbinu za ikolojia hutoa suluhu za muda mrefu zinazoweza kupanuliwa.
- Uadaptishaji wa ndani unaochanganya maarifa ya jadi na teknolojia bunifu hutoa njia za kuhimili mabadiliko.
- Uwekezaji wa kisera na kifedha ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji imara, usimamizi jumuishi, ushirikiano wa mipakani, na fedha za tabianchi unahitajika ili kukabiliana na changamoto hizi.
Milima ya Altai, Mongolia ya Magharibi.
Washindi wa Tuzo ya Mountain Future
Washindi wa Tuzo ya milima “Mountain Future” wametangazwa, wakitambua miradi bunifu inayojenga mnepo dhidi ya athari za kuyeyuka kwa barafu na kuimarisha uchumi na riziki za milimani.
Washindi hawa katika kategoria za ubunifu, urekebishaji, na vijana watapata ufadhili wa kuanzia kwa ajili ya kutekeleza miradi yao, pamoja na kutambuliwa na kuongezewa mwonekano.
Kundi la ubunifu
Aziz Soltobaev kutoka Internet Society Kyrgyzstan Chapter ametambuliwa kwa mradi wa gharama nafuu wa ufuatiliaji wa tabianchi unaotoa taarifa za wakati halisi kuhusu hali ya hewa na barafu kwa maeneo ya milimani.
Mradi huu unatumia vitambuzi vya bei nafuu na teknolojia ya mawasiliano ya umbali mrefu, unawafunza vijana kutumia zana za AI, na kuweka data yote wazi kwa umma.
Kundi la urekebishaji
Marcela Fernández na Estefanía Angel Villanueva wa Cumbres Blancas wametuzwa kwa mradi wao wa kurejesha mazingira ya milima nchini Colombia, unaoharakisha urejeshaji wa mimea ya frailejón na spishi nyingine asilia kwa kuchanganya uzalishaji wa maabara (in vitro) na vitalu vya jamii.
Pia unakuza uwezo wa vijana na jamii za asili huku ukilinda mifumo ya ikolojia inayotoa sehemu kubwa ya maji safi nchini humo.
Kundi la Vijana
Ali Sarwar kutoka Gulmit Educational & Social Welfare Society nchini Pakistan ameshinda tuzo hii kwa mradi unaowawezesha vijana kuongoza juhudi za ufuatiliaji wa barafu na maji katika Bonde la Gulmit. Vijana wanapewa mafunzo ya matumizi ya drones, ramani za GIS na vitambuzi vya kufuatilia hatari za mafuriko.
Mradi huu unahusisha vijana 100, ambao nusu ni wanawake, na unalenga kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga pamoja na kukuza ujuzi unaochochea ajira na ujasiriamali.
Wawakilishi kutoka Kyrgyzstan, Uswisi, Italia na Peru walihudhuria hafla hiyo, ambayo pia ilijumuisha vipindi vya majadiliano kuhusu vijana, maonesho ya picha yenye kichwa “On the Trail of the Glaciers”, na maonesho ya vyakula vya milima kutoka kwa wazalishaji wa Slow Food wa maeneo ya milima ya Italia.