
Tarehe 9 Desemba kwa kawaida huwa siku ya sherehe na faraja kwa Watanzania. Ni siku ya kukumbuka safari ya uhuru, mafanikio yake na changamoto zilizovukwa kwa kipindi chote cha uhuru wa nchi. Hata hivyo, mwaka huu hali ilikuwa tofauti kabisa.
Badala ya kuwa siku ya furaha mwaka huu kulitanda hofu. Badala ya shamrashamra, kulikuwepo ukimya uliotamalaki katika miji na majiji. Serikali ilitangaza wazi: “Wasio na shughuli za msingi washerehekee wakiwa nyumbani.”
Tangazo hilo lilikuwa wazi, lakini mantiki yake ilitokana na hofu ya kile kilichotajwa mitandaoni maandamano yasiyo na kikomo. Vijana kadhaa katika majukwaa ya mtandaoni walitangaza kwamba Desemba 9 ingekuwa mwanzo wa maandamano endelevu, na tayari walikuwa wametaja tarehe nyingine kuwa ni Desemba 25.
Katika mazingira ya kisiasa na kijamii ambayo bado hayajapona baada ya kile kilichotokea Oktoba 29, 2025 siku iliyoshuhudia vifo, uharibifu wa mali na vurugu zilizoacha alama mbaya hofu ilienea kwa kasi.
Matokeo yake, Watanzania wengi walibaki majumbani, wakihofia kupata madhara. Kwa neema ya Mungu, maeneo mengi nchini yalibaki shwari, lakini gharama ya hali hii ilikuwa kubwa kuliko tunavyoweza kudhani.
Vyombo vya ulinzi viliongeza ulinzi wa kiwango cha juu. Barabarani kulikuwa na vizuizi kila kona, safari zikawa ngumu, na usafiri wa kutoka eneo moja kwenda jingine ukawa mtihani. Vizuizi vya barabarani kila kona ili upite ulihitaji kuwa na kitambulisho wapo waliozuiwa kuendelelea na safari. Dar es Salaam jiji lisilolala lilikuwa kimya kiasi cha kushtua.
Video moja iliyosambaa mtandaoni ilionyesha madereva wa malori ya chakula wakilalamika kuzuiwa jijini, walikumbwa na hofu ya bidhaa zao kuharibika. Kwangu mimi tukio hilo lilikuwa zaidi ya habari ya mtandaoni; lilionyesha namna mnyororo mzima wa uchumi unavyoweza kuyumba kwa siku moja tu ya tahadhari.
Wafanyabiashara wadogo ndio walioumia zaidi. Maduka mengi yalifungwa. Wale wanaoishi kwa kutegemea kipato cha siku kwa siku machinga, bodaboda, mama lishe, wauza bidhaa za mtandaoni walijikuta katika hali ya sintofahamu.
Ni vigumu kufikiria mtu ambaye anategemea elfu tano au kumi kwa siku ili aishi, halafu siku hiyo ikawa hakuna mlango wa kufungua. Bila shaka walilala wakiwa na mawazo mazito.
Hofu ilijenga tabia nyingine pia. Siku kadhaa kabla ya Desemba 9, madukani kulifurika watu wakinunua vitu muhimu kwa wingi husuani vyakula. Ilikuwa kama tukio la “panic buying” kwa kimombo. Mitandaoni, watu walitaniana wakisema, “Kila nyumba imegeuka kuwa genge.”
Utani huo ulikuwa na ukweli mchungu ndani yake, kwani bidhaa muhimu zilipanda bei kwa sababu ya ongezeko la mahitaji. Na kama tunavyojua, bei ikishapanda si rahisi kurudi haraka katika hali ya kawaida.
Kwa ujumla, Desemba 9 ilisimamisha maisha kwa namna ambayo hatukuwahi kuzoea. Uchumi ulitetereka kwa masaa kadhaa na ikiwa tutaendelea na “maandamano endelevu” kila siku inayotajwa, basi tutashuhudia maisha yanayosimama mara kwa mara hali ambayo nchi haiwezi kuivumilia.
Na hapa ndipo hoja yangu ilipo, katika hili tusitafute mshindi kana kwamba huu ni mchezo wa msukumo na mvutano. Wapanga maandamano hawashindi kwa sababu uthibitisho wa madai yao haufiki pale wanapotamani, na jamii yenyewe inaumizwa.
Wanaoyazuia maandamano nao hawashindi kwa sababu gharama ya kiusalama, kiuchumi na kijamii inaendelea kupanda. Mwisho wa siku, anayeumia ni Mtanzania wa kawaida mchuuzi, dereva, mfanyakazi, mtoto anayetegemea kifungu cha mlo nyumbani.
Tunahitaji mjadala wa kitaifa. Tunahitaji kusikia hoja zote, malalamiko, hofu, matarajio na masuluhisho. Serikali ina wajibu wa kuongoza mazungumzo haya kwa busara na weledi.
Vijana na wanaharakati pia wana wajibu wa kuwasilisha madai yao kwa njia salama na yenye kujenga, bila kuweka maisha ya watu hatarini. Viongozi wa dini, mashirika ya kiraia na wazee wenye busara wana nafasi muhimu katika kutengeneza njia ya kati.
Haiwezekani tuishi katika hofu kila baada ya siku chache. Haiwezekani kila tishio litufanye tufunge biashara na kukaa majumbani. Hatuwezi kuweka uchumi wetu rehani na kuwafanya wawekezaji watazame pembeni. Hatuwezi kuharibu utaratibu wa kijamii kwa utaratibu ambao hauna mwisho.
Suluhu ya kudumu inahitajika na inahitajika sasa. Maandamano yasiyoisha hayataleta matunda, na kuyazuia kwa kiwango kinachoathiri maisha ya wengi hakutasaidia pia. Tanzania ni nchi ya amani, nchi ya majadiliano. Kama kuna wakati tunahitaji kuikumbuka misingi hiyo, basi ni sasa.
Maana yake ni moja tu: Hakuna mshindi katika mvutano huu. Ushindi unaweza kupatikana tu pale tunapoketi, kusikilizana na kuamua njia ya pamoja. Amani yetu ni muhimu kuliko ushindi wa pande moja.