Kampuni ya Amsons Group ya Tanzania imetangaza uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme wa jua wenye uwezo wa Gigawati 1 (1,000MW) nchini Zambia.

Uwekezaji huo ni sehemu ya mpango mpana wa nishati wenye thamani ya Dola milioni 900, unaojumuisha pia uzalishaji wa Megawati 300 za umeme wa makaa ya mawe.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Amsons Group, mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Amsons Group na kampuni ya Exergy Africa Limited ya Zambia, kupitia umoja wa wawekezaji wa nishati jadidifu – Africa Power Generation.

Makubaliano ya mradi huo yamesainiwa Ikulu ya Zambia, yakishuhudiwa na Rais Hakainde Hichilema, ambaye amesema mradi huo ni mabadiliko ya kwenye uwezo wa nchi kuzalisha nishati safi na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya umeme vinavyoyumba wakati wa ukame.

Serikali ya Zambia imesema uwekezaji huo unaonesha nguvu ya ushirikiano wa sekta binafsi katika kupunguza pengo la nishati na kuimarisha usalama wa gridi ya taifa.

Kwa mujibu wa Exergy Africa, mradi huu unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya FDI katika sekta ya nishati Kusini mwa Jangwa la Sahara na utaongeza uthabiti wa nishati kwa makazi, viwanda na huduma za kijamii.

Uwekezaji huu unakuja muda mfupi baada ya Amsons Group kuimarisha nafasi yake kwenye sekta ya miundombinu Afrika Mashariki kwa kununua kampuni ya Bamburi Cement nchini Kenya na kuongeza hisa katika katika kampuni ya East African Portland Cement (EAPC).

Kampuni hiyo sasa inafanya shughuli katika nchi tano za Tanzania, Kenya, Msumbiji, DR Congo na Zambia.

✍ @claud_jm
#AzamTVUpdates

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *