WAKATI wowote kuanzia leo Simba itamtangaza kocha mpya wa kigeni, atakayekuja kuchukua mikoba ya Dimitar Pantev aliyeachana na klabu hiyo kwa makubaliano ya pande hizo mbili, huku akiachiwa msala wa kufanya usajili dirisha dogo baada ya kukisoma kikosi kilivyo.
Simba imekuwa ikisimamiwa na Seleman Matola anayekaimu ukocha mkuu kwa sasa tangu aondoke Pantev aliyetambulishwa kama meneja wa klabu hiyo na kudumu klabuni hapo kwa siku 61 tu, akipigiwa kelele na mashabiki na wapenzi wa Msimbazi hasa baada ya kuishuhudia Simba ikilala mabao 2-0 mbele ya Azam FC.
Hata hivyo, ishu ya kocha Matola ilidaiwa kuwagawa mabosi na maazimio ya kikao ni kwamba kocha mpya wa kigeni aletwe fasta akiwa na wasaidizi wake, ili kuanza kazi mara moja kabla ya timu kurudia katika mechi za mashindano mbalimbali ya msimu huu.
Ipo hivi. Juzi Jumatano, mabosi wa Simba waliitana na kufanya kikao kizito cha pamoja kilichohusisha vigogo, lengo kubwa ni kujadili mchakato wa kocha wa kumrithi Pantev sambamba na kuunda benchi zima la ufundi ambalo awali lilikuwa likiongozwa na Mbulgaria huyo aliyeondoka na Matola mbali na mikakati mingine ya kuimarisha kikosi hicho ili kurudi katika mstari ulionyooka.
Simba ilivurugana baada ya kupokea vipigo viwili mfululizo vya mechi za awali za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali na kumtemeshea kibarua Pantev nakuiacha timu kwa Matola aliyeiongoza katika mechi mbili za Ligi Kuu ikiwamo ya Mbeya City iliyowafunga mabao 3-0 kisha kupoteza kwa Azam Fc kwa mabao 2-0.
Mwanaspoti linafahamu, kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kimebariki ujio wa kocha mpya wa kigeni na kubadilisha benchi hilo, lakini Matola bado ataendelea kuwepo.
Mabosi wa Simba wameshindwa kukubaliana na wazo ya kutaka kumwachia jumla Matola benchi hilo la ufundi, kwa kuamini haitakuwa na afya njema kwa kikosi hicho kwa sasa na kwamba kocha mpya watakayemalizana watamtangaza muda wowote kuanzia sasa.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kimelidokeza Mwanaspoti, licha ya Matola kuungwa mkono na mabosi walio wengi walioshiriki kikao hicho, lakini mwenyewe alikuwa akishinikiza aachwe akapate changamoto nyingine nje ya Msimbazi, huku mabosi wakitaka asalie kama msaidizi wa kocha mpya ajaye, japo msimamo wa mwisho umeshindwa kuwekwa bayana na chanzo chetu kilichoteta na Mwanaspoti jana.
Imedaiwa, bodi hiyo imetaka uongozi wa Simba kuharakisha mchakato wa kocha mpya, ili awahi kuanza maandalizi ya timu kabla ya mechi za mashindano kuendelea mapema mwakani.
Simba ipo Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika ikishika mkia bila pointi kwa sasa nyuma ya Esperance ya Tunisia yenye pointi mbili, huku Petro Atletico na Stade Malien zikiongoza kwa kila moja kuwa na pointi nne ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, lakini ikikabiliwa an mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) linalotarajiwa kuanza mechi za awali hivi karibuni.
“Tumekubaliana tutafute kocha mpya, kwani timu yetu ilipofika ni lazima tutafute kocha mwenye uwezo mkubwa kuliko huyu kocha aliyepita,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka Simba.
“Mchakato huu siyo kuanza tu, bodi imeagiza utimie haraka. Unajua matokeo tuliyoyapata hapa kati yamewamumiza wengi na tunataka apatikane kocha atakaye badilisha hili na awe wa maana kweli siyo kama huyu aliyepita ambaye tunadhani uchaguzi wake ulifanyika kwa kutopima mambo mengi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kwa ishu ya Matola, tuiache kwanza, ila ni kwamba kikao kimegundua tatizo la Simba wala sio Matola. Kuna mambo mengi yaliyochangia timu kufika hapo tulipo,” kilisema chanzo hicho.
Miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kupewa shavu ni Msauzi Steve Becker na Antonio Casano wa Hispania.
MSALA WA USAJILI
Kikao hicho kilikubaliana pia hatua ya usajili isubiri ujio wa kocha mpya kuangalia ubora wa wachezaji kisha atashauri nini kifanyike.
“Usajili utasubiri kocha mpya afike tumsikie ushauri wake kulingana na wachezaji atakaowaona, ndiyo maana pia tumeagiza aje mapema awaangalie wachezaji alionao ili ukifika wakati wa usajili kama atahitaji watu tutajadiliana naye.”
Hata hivyo, licha ya chanzo hicho kuweka bayana usajili wa dirisha dogo utategemea uamuzi wa kocha mpya, lakini tayari kuna majina kadhaa ya wachezaji wanaopigiwa hesabu ambayo yalipendekezwa na Pantev, sambamba na wale watakaotolewa ikiwamo wa mkopo kwa lengo la kuiimarisha Simba.
Ligi Kuu kwa sasa imesimama hadi Januari kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 itakayofanyikia Morocco kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani na Tanzania inashiriki.