Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Msaada wa Dharura OCHA, imesema hali katika jimbo la Kivu Kusini imezorota kwa kasi tangu tarehe 2 Desemba kutokana na mapigano mazito katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Uvira, Walungu, Mwenga, Shabunda, Kabare, Fizi na Kalehe.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, wanachama wa kundi la waasi la M23 waliingia katika jiji muhimu la Uvira jana Jumatano na wakazi wameripoti hali ya hofu na kutojiamini.
Radio Okapi, inayosimamiwa na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, imeripoti kuwa zaidi ya raia 74 wameuawa na angalau 83 kujeruhiwa katika mapigano kati ya vikosi vya Congo na makundi yenye silaha tangu mapema mwezi Desemba. Redio hiyo imesema maelfu zaidi wamekimbilia nchi jirani za Burundi na Rwanda.
Wengi wa waliokimbia ndani ya Kivu Kusini wanahifadhiwa katika maeneo yaliyofurika watu, wakikabiliwa na hatari kubwa za ulinzi, usafi duni na tishio linaloongezeka la milipuko ya magonjwa. Wanawake na wasichana waliokimbia makazi wanakabiliwa na hatari zaidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo hayo yenye msongamano.
Watu waliokimbia makwao kutokana na ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanapokea msaada.
Msaada wa chakula wasitishwa
Mipango ya misaada ya kibinadamu, ikiwemo msaada wa chakula na huduma za afya, imeathiriwa na ukosefu wa usalama.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha shughuli zote katika jimbo la Kivu Kusini, na hivyo kuwakata kwenye msaada wa chakula unaookoa maisha watu 25,000, kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq.
“Familia zinazowahifadhi wakimbizi, ambazo tayari zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, zinagawana chakula chao cha mwisho na watu waliokimbia makazi,” amewaambia waandishi wa habari jijini New York.
Takriban shule 32 mjini Uvira zinazosaidiwa na WFP zimesitisha masomo ili kuhifadhi familia zilizoikimbia makazi, na hivyo kuwaacha zaidi ya watoto 12,000 bila mlo wao pekee wa moto wa kila siku.
Mashirika ya kibinadamu yameonya kuwa akiba ya chakula katika eneo hilo inaweza kuisha ndani ya wiki chache ikiwa ufikiaji na ufadhili hautarejeshwa.
Watu wanaendelea kukimbia ghasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Hofu ya kuvuka mipaka yaongezeka
“Athari za kibinadamu za mgogoro huu sasa zinavuka mipaka,” amesema Bwana Haq, akiripoti kuwa karibu watu 25,000 walivuka kuingia Burundi kati ya tarehe 5 na 8 Desemba, huku idadi zaidi ikiripotiwa kuingia Rwanda.
Katika nchi zote mbili, mashirika ya kibinadamu na mamlaka za kitaifa zinaongeza misaada ya dharura, ikiwemo milo ya moto, maji safi na huduma za afya.
Mvutano huu umeongezeka licha ya jitihada za kidiplomasia kupunguza hali ya ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.
Wiki iliyopita, DRC na Rwanda zilisaini makubaliano ya amani yaliyosaidiwa na Marekani, ambayo Umoja wa Mataifa uliyataja kuwa “hatua muhimu ya kurejesha uaminifu.”
Changamoto za ufadhili zaongeza mgogoro
Upungufu wa ufadhili unachochea dharura hiyo. Mpango wa hatua za Kibinadamu wa DRC umefadhiliwa kwa asilimia 22 pekee, na kuacha pengo la karibu dola bilioni 2, ameonya Bwana Haq.
Huko Burundi, chini ya dola milioni 33 zimepatikana kati ya mahitaji ya karibu dola milioni 77 kuwasaidia wakimbizi wapya.
“Tunaziomba pande zote zinazohusika na mgogoro kusitisha mapigano mara moja, kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kulinda raia na miundombinu ya kiraia, na kuhakikisha upatikanaji salama, wa haraka na usio na vikwazo kwa misaada ya kibinadamu,” amesema.