
Wakati Bongo Fleva inaanza kuja kasi, sehemu kubwa ya jamii iliuona ni kitu cha kihuni, ilipigwa vita haswa na madingi. Wazazi hawakutaka watoto wao kufanya huu muziki.
Miaka ya 2000 hali ikabadilika. Bongo Fleva ikateka kila kitu na kila mtu, ikawa na nguvu kuliko chochote. Hakuna tukio kubwa bila muziki huu, kuanzia Kimara na Tandika hadi Kakamega na Kibera.
Shughuli zilizohitaji kuwavutia watu wengi. Matamasha binafsi au ya serikali, kampeni maalumu au matangazo ya kibiashara. Ni wasanii wa muziki huu waliotumika zaidi. Hivyo ile dhana ya uhuni ikafutika kabisa kwenye vichwa vya watu. Hata wazazi wakaanza kutamani kuwa na watoto ambao ni wasanii kwa sababu waliona matunda yake.
SANAA NA SIASA
Jakaya Kikwete, aligombea urais kwa mara ya kwanza 2005. Ndipo siasa ilipouteka rasmi huu muziki. Jakaya maarufu kama JK alipendwa sana na vijana, na kampeni zake zikabebwa na muziki huu wa vijana.
Haikuwa bahati mbaya kutumia Bongo Fleva. Watu waliupenda muziki na wanamuziki wake, ili kuhalalisha jambo lako livutie watu wengi, hakukuwa na namna ya kuukwepa muziki huu.
MUZIKI HADI IKULU
Ni Jakaya aliyewapa heshima wasanii na kuigeuza Magogoni kama studio za P Funk. Waliingia kila mara na kuheshimiwa kutokana na mchango mkubwa waliotoa kwenye kampeni.
Ngwair licha ya kumpamba na kumsifu Jakaya kwa kumtungia wimbo wa ‘Mtoto wa Jakaya’. Baada ya kampeni kumalizika hakuna aliyemchukia Ngwair. Na maisha yakaendelea huku dogo akiendelea kukusanya kijiji chake kila anapopiga shoo.
Wanaume TMK, walitumika kwenye kampeni za mwaka 2005, wakatumika 2010 na wakatumika tena 2015. Lakini, hakuna kelele wala vinyongo kwao na maisha yakaendelea. Wasanii walirudi kwenye sanaa yao kiroho safi. Unajua kwa nini?
Mwaka 2020, Diamond, Kiba na wengine walishiriki kampeni za Hayati Magufuli, tena kukiwa na hasira nyingi kwa wapinzani. Kutokana na madudu yaliyotokea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.
Sitaki kuingia sana huko kwa sababu kila mwenye macho aliona uchaguzi ulivyokuwa.
Baada ya kampeni ya 2020, tena kukiwa na wasanii wa filamu pia. Hakukuwa na kelele kwa wasanii wala kususiwa kazi zao achana na vitisho. Wasanii walioshiriki kampeni waliishia kuitwa chawa bila kususia kazi zao na maisha yakaendelea.
CHUKI YA WAZI
Kwanini 2025 hali imekuwa hivi? Ni kwa sababu baadhi ya wasanii walivuka mipaka. Wakaacha kazi ya kuwapamba wagombea wao wakaanza kuwadhihaki na kuwatusi wananchi ambao ndio wateja wakubwa wa kazi zao.
Hawa wananchi ndio wanatoa fedha wanazozipata kwa kuvuja jasho na damu kulipa viingilio kwenye shoo, kununua ngoma zao kwenye vibanda vya video wakiwa na flash zao. Hili lilikuwa kosa kubwa sana.
Ile video ya Diamond, Dimpoz na Jux wakionekana kuwananga wananchi kwamba, waache kulialia wafanye kazi. Kwamba kila mtu acheze mechi zake na mitusi juu. Lilikuwa kubwa kwa mashabiki na wananchi kwa ujumla.
Hasira zote hizi za wananchi juu ya wanamuziki wote, hawa ndiyo chanzo. Hakuna raia aliyekuwa na hasira na msanii ambaye anatafuta maisha na mkate wake kupitia kampeni za siasa.
Mpaka baada ya kauli za kina Mondi. Miaka yote wasanii wanatumika kwenye majukwaa ya siasa, lakini hakuna hasira wala chuki dhidi yao.
WEMA NAYEE…
Miongoni mwa wasanii waliolizua na kulipalilia kama si kulipaka mafuta na kulipua hasira za mashabiki na wananchi ni pamoja na Wema Sepetu. Juzi kati mlimbwende huyo akawashukia Gen Z baada ya kumkalia kooni. Aliwasuta na kuwananga kisha akawaambia wamkome kabisa.
Kauli ya Wema Sepetu kusema Gen Z wamkome ni kachumbari tu, lakini msosi kamili ni maneno na matusi ya Mond, Dimpoz na wenzake. Kwamba watu waache kulialia wafanye kazi.
Waliposema wao wanafanya kazi sana ndo maana wana magari ya kifahari. Wakisahau kwamba hao hao ndo wapiga kura wa tuzo zao, wanunuzi wa tiketi za shoo na pia ‘masabuskraiba’ wao. Hili lilikuwa kosa la kiufundi. Yaani hapa ndio walianza kuchoma picha.
Wengi mitandaoni wanarudia kauli zao kwamba, wasanii nao waache kulialia wafanye kazi. Ni wazi wengi walikerwa na kauli za majivuno, kebehi na dhihaka za Mond na wenzake.
FAMILIA ZIWE NA BREKI
Wakati Jizzo akiwaombea radhi kina Diamond, mama yake Mond akaliamsha dude huko. Kwamba mtoto wake hategemei muziki ili kuishi. Hapa alikuwa akiwananga kiaina Gen Z.
Hii ni shida ya familia zetu kukosa breki na maneno sahihi ya kuzungumza katika wakati sahihi. Hata asipotegemea muziki kwa maisha yake yaliyobakia duniani.
Lakini, hili tatizo siyo kwa msanii mmoja tu, bali ni tasnia ya muziki dhidi ya walaji wa kazi za muziki. Hapo Mond alipofika kwa sababu ya hawa tunawaambia watukome, waache kulialia wafanye kazi na hatutegemei mziki kuendesha maisha. Hawa ndio walichonga barabara za mafanikio ya wasanii wote hivyo, baada ya kupita kuanza kuwananga na utovu wa nidhamu na kukosa shukurani.
MUZIKI NA SIASA
Kushiriki kampeni za uchaguzi kwa wanamuziki siyo kosa kwa sababu ni sehemu ya kazi kama zilivyo zingine. Na kuegemea upande kwenye hizi siasa pia siyo kosa. Kosa ni pale tunaposhindwa kutumia ndimi zetu kwa usahihi katika wakati sahihi. Wasanii wana mashabiki katika vyama vya siasa karibu vyote na hata wale wasio na vyama hivyo, wanapokuwa upande fulani kauli zao ndio zinabaki kuwa silaha kubwa kwa kesho yao.
Hata wanasiasa wenyewe pale wanapotumia vibaya ndimi zao ‘huwakosti’. Mpambe mgombea umtakaye utakavyo bila dhihaka dhidi ya mgombea ama chama kingine. Kwa sababu msanii ni wa wote, una mashabiki hata upande ule usioutaka.
NINI CHA KUFANYA?
Majizzo kaleta mjadala wa nini kifanyike ili kutoka kwenye huu mkwamo. Lakini, alichofanya ndilo jibu sahihi, tatizo ni kwamba alitoka kivyake kuwaombea radhi watu wazima ambao, wenyewe hawajataka kutubu hivyo ni sawa na kuwa hajakubali kama wamefanya makosa.
Wengine ni maboss wa vituo vya radio kama yeye. Jizzo alipaswa kuibuka na Diamond, Dimpoz na wenzao na kuitisha ‘presi’ kisha awaombee radhi wakiwepo na wenyewe waombe radhi pia.
Hii ni kama Majizzo alijitafutia eneo lake tu vijana wa kileo wanasema anajipendekeza ama kajituma ama anatafuta sifa na ushindi wa mezani.
Wasanii wetu wanapaswa kutambua kwamba, wakati wakitamba kwa maneno ya dharau na dhihaka kwamba, wana pesa na magari ya kifahari wakumbuke kina watu waliteseka kuuweka huu mziki kwenye ramani.
Hawa kina Mondi, Dimpoz na wenzake wamekuja kuteleza baada ya kuwa kina Sugu, Profesa Jay, P-Funk, Master J, James Dandu na wengine walishachonga barabara na kuweka lami. Hawa walifanya kazi kubwa kuaminisha jamii kwamba, muziki huu ni fursa, ni ajira na unaongeza upeo na sio uhuni kama walivyodhani. Wanapaswa kuendesha mambo kwa nidhamu ili wapande mbegu kwa ajili ya vizazi vijavyo.