Dar es Salaam. Serikali imesema usaili wa ajira mpya 12,000 za afya na ualimu, utaanza rasmi kesho Jumamosi Desemba 13,2025 katika mikoa ya Tanzania bara na vituo mahususi vya Unguja na Pemba.

Sambamba na hilo, Serikali imeeleza kuwa hadi kufikia Januari 2026, mchakato huo utakuwa umekamilika na kila aliyefaulu kwenye mchujo atapangiwa kituo chake cha kazi.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 12, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na wanahabari kuhusu wizara hiyo ilivyojipanga kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2025/26.

“Katika mwaka 2025/26 Serikali imefanikiwa kutoa kibali cha nafasi 41,500 za ajira zikiwemo 12,000 ambazo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoahidi na imeandikwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” ameeleza Ridhiwani.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, Rais Samia aliahidi ajira 12,000, kati ya hizo 5,000 za afya na 7,000 ualimu (masomo ya sayansi na hisabati) akisema itatekelezwa ndani ya siku 100 baada ya kushika madaraka.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, usaili utafanyika kwa kila ngazi ya mkoa, hivyo waombaji hawatalazimika kwenda Dodoma, kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Aidha Waziri huyo amesema ili mchujo ufanyike kwa wakati na kuongeza ufanisi, usaili wa mchujo wa nafasi hizo utafanyika kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ‘Online Aptitude Test (OATS).

“Utafanyika katika vituo mbalimbali ikiwemo taasisi za elimu ya juu, Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi (Veta) na shule za sekondari zenye maabara za kompyuta zinazopatikana katika mikoa yote na vituo vya Unguja na Pemba,”

“Niwaombe waombaji wa nafasi hizi, kuangalia kwenye akaunti zao za mfumo wa ‘Ajira Portal’ ili kujua vituo walivyopangiwa kwa ajili ya usaili,” amesema Waziri Kikwete.

Waziri huyo, amewataka waombaji wote walioitwa kwenye usaili kuhakikisha wanabeba nyaraka zote muhimu, ikiwemo vyeti vyao ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza.

“Mungu akitujalia heri mchakato huu tutaukamilisha Januari 2026. Kwa kasi iliyoanza pale wizarani kabla ya siku 100 za Rais Samia hazijaisha, tutakuwa tumekamilisha, na waombaji watajulishwa kwa mfumo kuhusu vituo vya kazi watakavyopangiwa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete amesema Serikali imefanya maboresho mfumo wa kutoa maoni, ‘e-Mrejesho’, ili kuwezesha wananchi kueleza malalamiko na hata pongezi kuhusu huduma zinazotolewa Serikalini na taasisi zake.

Pia, Waziri Kikwete amesema wizara hiyo, imejenga mfumo wa kielektroniki wa Daftari la Huduma za Serikali ili kuimarisha mifumo ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

“Lengo la kuanzisha Daftari la Huduma za Serikali ni kuongeza ufanisi na uwazi katika taarifa zote za huduma kuanzia michakato ya huduma hadi gharama,” amesema Waziri Kikwete.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *