Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka kipaumbele katika ajenda ya ustawi na mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza huduma za malezi mbadala, usimamizi wa Makao ya Watoto nchini ili kuhakikisha yanatoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa ziara ya kutembelea Makao ya Watoto ya Taifa Kikombo Jijini Dodoma na kujionea huduma zinazotolewa katika Makao hayo.
Mhe. Maryprisca amesema Makao ya Taifa ya Kikombo ni mfano wa Taasisi ya Serikali inayotekeleza majukumu hayo kwa weledi, upendo na dhamira ya dhati.
“Nimetembelea miradi, miundombinu na kupokea taarifa ya mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuimarishwa, nafurahishwa kuona jitihada kubwa zinazofanywa katika kutoa huduma ya Elimu, Afya, Lishe, ushauri nasaha pamoja na malezi kwa Watoto napenda kuwahakikishia kuwa Wizara itahakikisha Makao haya yanawezeshwa ipasavyo”. amesema Mhe. Maryprisca.
Aidha Mhe. Maryprisca ametoa rai kwa wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kuendelea kushirikiana na Wizara kwa kuwapa watoto fursa sawa za maendeleo kama ilivyo kwa watoto wengine wote wa Tanzania.
“Niwaombe Mashirika, wadau wa maendeleo tuendelee kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza makazi ya watoto ili wawe na huduma nzuri na wasijione wanyonge na niwaambie kuwa ninyi ni watu muhimu, mnapendwa na Taifa linawahitaji, msipoteze matumaini, someni kwa bidii, zingatieni maadili, muwe na nidhamu na mtumie fursa mnazopata ili mkafikie ndoto zenu.”
amesema Mhe Maryprisca