Akizungumza na Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa UNIS Nairobi kandoni mwa Kikao cha 7 cha Mkutano wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA-7 unaofunga pazia leo, Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP barani Afrika, Dkt. Richard Munang, anasema bara lhilo imepiga hatua, lakini si kwa kiwango kinachohitajika.

Dkt. Munang amesema Afrika inaendelea kukumbwa na majanga ya tabianchi, na kuongezeka kwa uhaba wa chakula. Licha ya miongo mitatu ya mazungumzo ya kimataifa, anasema mamilioni ya Waafrika bado wako mstari wa mbele wa athari za tabianchi.

“Ukame haujasimama, mafuriko hayajakoma, na leo usiku zaidi ya Waafrika milioni 278 watalala njaa.”

Amesisitiza kuwa hiyo ndio hali halisi. Hata hivyo, Dkt. Munang anaangazia hatua muhimu zilizopigwa hadi sasa. Karibu nchi zote za Afrika zimeridhia Mkataba wa Paris, nyingi zimepitisha sheria za tabianchi na kuandaa mipango ya kitaifa ya hatua za kukabiliana na tabianchi. Sheria ya Tabianchi ya Kenya ya mwaka 2016 ni amesema ni mfano wa nchi zinazoongoza mabadiliko yao ya kijani.

Mabadiliko makubwa ya misimu ya mvua kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa kilimo na maisha ya jamii .

© Unsplash/Bogomil Mihaylov

Mabadiliko makubwa ya misimu ya mvua kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa kilimo na maisha ya jamii .

“Asilimia zaidi ya 98 ya nchi za Afrika zimeridhia Mkataba wa Paris. Hayo ni maendeleo halisi. Bara limeonesha kuwa linafahamu fursa zinazotokana na kuchukua hatua kuhusu tabianchi za kiuchumi, kiafya na ajira  kwa vijana”

Lakini ameonya kuwa changamoto kuu, ni kutafsiri ahadi kuwa matokeo ya kweli, matokeo yanayolinda maisha, kujenga mnepo, na kufungua milango ya ukuaji wa uchumi unaojali mazingira.

Munang anasisitiza kuwa muongo ujao lazima ulenge kwa kasi katika kuongeza utekelezaji na si maneno matupu akisistiza kuwa Pengo katika miaka hii kumi halikuwa sera, Afrika ina sera.

“ Pengo limekuwa kuzigeuza sera hizo kuwa uhalisia. Tunachohitaji sasa ni utekelezaji, utekelezaji na utekelezaji.”

Wakati Mkataba wa Paris unafikisha miaka kumi, Dkt. Munang amesema Afrika iko katika mwendo wa kati, ikikabili hatari kubwa lakini pia fursa kubwa zaidi. Changamoto sasa, anasema, ni kuhakikisha kuwa utashi wa kisiasa unaendana na hatua za kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *