
Azimio hilo, lenye kichwa “Kukuza Suluhu Endelevu Kupitia Michezo kwa Ajili ya Sayari yenye mnepo,” linathibitisha tena maamuzi ya awali ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yanayotambua nafasi ya michezo katika kuhimiza elimu, afya, amani na maendeleo endelevu. Pia linakumbusha kazi ya muda mrefu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kushirikiana na mashirika ya michezo katika kusukuma mbele hatua za kimazingira.
Nchi wanachama zimeangazia jukumu la michezo katika kuimarisha ujumuishaji wa kijamii na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya mazingira, huku zikikiri pia hitaji la kupunguza athari hasi za kimazingira zinazotokana na matukio makubwa ya michezo na miundombinu yake.
Kupitia azimio hilo, wanazisihi serikali kuingiza masuala ya uendelevu katika mikakati ya kitaifa ya michezo, mitaala ya elimu ya mwili, na programu za michezo za kijamii. Mataifa pia yanahimizwa kuzingatia hatua kama vile usimamizi endelevu wa matukio ya michezo, ujenzi wa miundombinu stahimilivu, usimamizi bora wa taka, na matumizi ya suluhu zinazotokana na maumbile.
Ikitambua uwezo tofauti wa nchi, UNEA-7 imeitaka jamii ya kimataifa kuongeza msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kutekeleza kikamilifu miradi ya michezo endelevu.
Azimio hilo pia linamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP kusaidia nchi zinazovutiwa kwa kuandaa vifaa vya elimu, kuongeza mnepo wa umma na kujenga uwezo wa mashirika ya michezo na mamlaka za mitaa. UNEP imeombwa pia kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa mazingira na jumuiya ya michezo duniani.
Zaidi ya hayo, UNEP itasasisha mkakati wake wa muda mrefu kuhusu michezo na mazingira ifikapo mwaka 2027, na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji katika kikao kijacho cha Baraza la Mazingira.
Uidhinishaji wa azimio hili unaonesha msukumo unaoongezeka kimataifa wa kutumia ushawishi mpana wa michezo katika kuunga mkono ulinzi wa mazingira na kuongeza uthabiti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.