“Kinachofahamika kwa sasa kuhusu hali ilivyo El Fasher ni cha kutisha kupita maelezo,” huyo ni Ross Smith, Mkurugenzi wa Maandalizi na hatua dhidi ya matukio ya dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) akizungumza kwa njia ya video na waandishi wa habari katika Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi Akieleza hali tete ya eneo la El Fasher nchini Sudan anafafanua zaidi akisema, “tunajua kwamba kuna kati ya watu 70,000 na 100,000 ambao huenda bado wamenaswa ndani ya mji wenyewe.”

Wanajeshi wa Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), ambacho kimekuwa kikipigana na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023, waliteka El Fasher, makao makuu ya mkoa wa Darfur Kaskazini  mwezi Oktoba mwaka huu, baada ya kuuzingira mji huo kwa siku 500.

Mateso hayo yaliwalazimu watu kula maganda ya karanga na chakula cha mifugo, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilionya wakati huo, huku picha za setilaiti zikionesha madoa ya damu yaliyosababishwa na mauaji ya halaiki ya raia na kuuawa kwa misingi ya kikabila.

Kupata fursa ya kuingia kwa timu za misaada bado ni jambo la dharura, mashirika ya kibinadamu yanasema, miongoni mwa changamoto ni kukatika kwa mitandao ambako kumezuia mawasiliano na wale waliobaki ndani ya El Fasher. Bwana Smith anaeleza kuwa ushuhuda wa walionusurika “unauelezea mji kama eneo la uhalifu lenye mauaji ya halaiki, miili iliyochomwa, na masoko yaliyoachwa wazi.”

Watoto ambao familia zao zilikimbia El Fasher wanasoma shule ya kijijini huko Tawila, Darfur Kaskazini.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Watoto ambao familia zao zilikimbia El Fasher wanasoma shule ya kijijini huko Tawila, Darfur Kaskazini.

Wito

“Tunatoa wito, na tumeendelea kutoa wito, kuruhusiwa kuingia El Fasher bila vizuizi ili kuwahudumia kwa dharura wale waliobaki wamenaswa mjini,” anasema Bwana Smith kwa niaba ya WFP na kwamba, “ninaelewa kutokana na mazungumzo ya jana kuwa tumefikia makubaliano ya awali na Rapid Support Forces kuhusu masharti ya msingi ya kuingia mjini; hivyo tunatarajia kuweza kufanya hivyo karibuni sana, kufanya tathmini za mwanzo na uchunguzi. Baada ya zaidi ya mwaka mmoja na nusu chini ya mzingiro, mahitaji muhimu ya kuishi yamefifia kabisa.”

Aidha Smith amebainisha kwamba wale walioweza kukimbia El Fasher wamehatarisha maisha yao katika barabara “zilizojazwa na mabomu ya ardhini na mabomu ambayo hayajalipuka.”

Misaada inaendelea Katikati mwa changamoto

Timu za misaada za Umoja wa Mataifa na wadau wanaendelea kushinikiza kupata fursa ya kuwafikia wote wanaohitaji; huku misafara inayosaidiwa na WFP, “ikiwa njiani kuelekea Tawila sasa, ikiwa na chakula cha kutosha kwa watu 700,000 kwa mwezi ujao,” amesema Smith akifafanua, “hizi ni familia ambazo zimestahimili njaa kwa miezi mingi mfululizo na ukatili mkubwa, na sasa wanaishi katika mazingira yenye msongamano mkubwa na msaada mdogo sana. Hakuna makazi ya kutosha, wengi wanaishi kwenye vibanda vya muda vilivyotengenezwa kwa nyasi na majani. Kipindupindu na milipuko ya magonjwa imesambaa.”

Sudan ndiyo nchi yenye janga kubwa zaidi la wakimbizi wa ndani duniani, ikiwa na zaidi ya watu milioni 12 waliokimbia makazi yao ndani na nje ya nchi.

Takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR zinaonesha kuwa zaidi ya watu 40,000 wamekimbia kutoka Kordofan Kaskazini tangu 18 Novemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *