Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx, leo imetangaza washindi wa droo ya kwanza ya kampeni yake ya mwisho wa mwaka, “Magift ya Mixx Pesa”, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwashukuru na kuwawezesha wateja wake nchini kote. Kampeni hii, ambayo ilizinduliwa tarehe Desemba 2, 2025, imeanza rasmi kuwazawadia watumiaji wa Mixx wanaofanya miamala mingi zaidi.

Akizungumza wakati wa kutangaza washindi, Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx, James Sumari, alisema kampeni hiyo inalenga kuwashukuru wateja wake lakini zaidi ni kuleta furaha kwa wateja hususani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na sikukuu ambapo mahitaji ya kifedha huongezeka.

“Tunatambua kuwa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, Watanzania wengi huwa na majukumu na mahitaji mbalimbali. Ndiyo maana tumeandaa kampeni rahisi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wateja wetu wapendwa,” alisema Sumari.

Sumari alibainisha kuwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ni rahisi, kwani mteja anachotakiwa kufanya ni kuongeza matumizi ya huduma za Mixx kama Lipa kwa Simu, ununuzi wa LUKU, kulipia maji, na huduma mbalimbali za kila siku. “Tunawahimiza wateja wetu kwamba huu ndiyo muda maalum wa kufanya miamala mingi zaidi ili kuingia kwenye droo ya ushindi. Leo tunaanza na washindi wa droo ya kwanza, lakini kampeni bado inaendelea. Tunawaalika wateja wote waendelee kushiriki ili nao waibuke na ushindi,” aliongezea.

Droo ya kwanza imetoa jumla ya washindi nane (8) ambao wametangazwa rasmi leo. Miongoni mwao ni mshindi wa jumla wa wiki, Bw. Ramadhani Bakari Sultan (42), fundi ujenzi na mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, aliyejishindia Sh5 milioni

Washindi wa zawadi za kila siku (milioni 1 kila mmoja) ni pamoja na Kutali Juma Nakumbya – Mkazi wa Dar es Salaam na Mjasiriamali, Abel Joseph Nyarubandwa (49) – Fundi Magari na mkazi wa Moshi, Jacqueline Julius Saye (33) – Mjasiriamali na mkazi wa Morogoro, Fatuma Mustapha Bujwera (62) – Mkazi wa Dar es Salaam, Mjasiriamali, Godbless Raymond Mbele (37) – Mjasiriamali na Mkazi wa Kagera, Joyce Edward Steven (31) – Mkazi wa Dar es Salaam na Mwalimu wa Chekechea, Happy Nicholaus Munuo (48) – Mjasiriamali na mkazi wa Temeke

Kwa upande wake, mshindi wa milioni moja, Joyce Steven, alisema hakuwahi kutarajia kushinda, lakini ushindi huo utamsaidia kutatua changamoto kadhaa za kifedha alizonazo.

“Namshukuru Mungu kwa ushindi huu. Nitazitumia pesa hizi kulipa kodi, ada ya mtoto na mambo yangu ya vikoba. Siri yangu imekuwa ni kufanya miamala mara kwa mara, kupokea pesa kama kijumbe na kulipia bili mbalimbali,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *