Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ameendelea kuonesha msukumo wa mageuzi ya kilimo nchini baada ya kuzindua miongozo mipya ya uzalishaji endelevu wa mazao muhimu kama ufuta, maharage, dengu, choroko, soya na mbaazi—miongozo inayosimamiwa na Mamlaka ya Uthibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na zaidi ya wataalam wa kilimo na ushirika 600 kutoka mkoa wa Lindi, ambapo Waziri Chongolo alisisitiza umuhimu wa miongozo hiyo katika kuboresha mnyororo wa thamani na kuongeza tija kwa wakulima.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, alisema miongozo hiyo itakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa, hatua itakayoongeza kipato kwa wakulima na kuimarisha kilimo biashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Rajab Telack, aliwataka watumishi wa umma katika mkoa huo kuanzisha mashamba ya mfano yatakayotoa elimu kwa wakulima na wakati huohuo kuwaongezea kipato chao.
Maafisa kilimo na ushirika nao walipongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa miongozo hiyo itawawezesha kusimamia vyema uzalishaji kwenye maeneo yao ya kazi na kuongeza ufanisi kwa wakulima.
Katika hatua nyingine, Waziri Chongolo alipata nafasi ya kutembelea maonyesho ya taasisi za kilimo yaliyoweka wazi teknolojia na mbinu bora za kilimo, ili kuwaongezea elimu maafisa ugani na wadau wengine wa sekta hiyo.
#StarTvUpdate