Taasisi ya Unicorn Allianz kuweka historia mpya! Tanzania inajiandaa kuandika ukurasa mpya katika historia ya diplomasia ya uchumi na uwekezaji barani Afrika, kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Unicorn Allianz State Summit (UASS).

Jukwaa hili la kimataifa la uchumi na uwekezaji linaratibiwa kwa ukaribu na Ofisi ya Rais, kupitia Wizara ya Uwekezaji na Mipango, chini ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum (TISEZA).

UASS ni mkutano mkubwa wa kwanza wa aina yake nchini, unaotarajiwa kuwa miongoni mwa majukwaa makubwa zaidi ya kiuchumi barani Afrika mwaka 2026. Mkutano huu wa kihistoria utafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, tarehe 17–18 Februari 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC). Tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na linaongozwa na kaulimbiu ya:-

“Kuchochea Uwekezaji Endelevu na Ukuaji wa Uchumi wa Tanzania kwa Miaka Mitano Ijayo kuelekea Kutimiza Dira ya Maendeleo 2050.”

Lengo kuu la UASS ni kuimarisha umoja wa kitaifa, ushirikiano wa kimataifa, pamoja na ukuaji wa uchumi na uwekezaji wa ndani na wa kigeni. Mkutano huu utatumika kama jukwaa la kimkakati la kujenga ubia, kubadilishana maarifa, na kujadili mwelekeo wa uchumi pamoja na maeneo mapya ya uwekezaji yatakayolifanya Taifa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.

UASS inatarajiwa kuwakutanisha pamoja Wizara zaidi ya 16 na Mawaziri wake, pamoja na takribani viongozi na watumishi wa Serikali zaidi ya 600.

Aidha, jukwaa hili linatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa wa kimataifa kwa kuwaalika Mabalozi zaidi ya 50, pamoja na wawakilishi wa mashirika makubwa ya maendeleo ya kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia (World Bank), Umoja wa Mataifa (UN), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na mengineyo.

Ushiriki wa wadau utakuwa mpana na wa kimkakati, ukihusisha wawekezaji zaidi ya 450 wa ndani na wa kimataifa, taasisi binafsi na za umma zaidi ya 500, pamoja na NGOs zaidi ya 250.

Majadiliano na fursa zitagusa sekta muhimu za uchumi zikiwemo Afya, Madini, Nishati, Viwanda na Biashara, Utalii, Kilimo, Teknolojia, Ujenzi na Miundombinu, Fedha na Bima, pamoja na Usafirishaji, jambo linaloonesha upeo, uzito na mvuto wa kimataifa wa jukwaa hili.

Kupitia UASS, Tanzania inatarajia kunufaika kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kimataifa, kuvutia mitaji mipya, kuonesha vivutio vya uwekezaji, na kuwakutanisha wadau wakuu wa maendeleo watakaotoa mchango wa moja kwa moja katika kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu.

Taasisi ya Unicorn Allianz inaamini kwa dhati katika nguvu ya Umoja wa Kitaifa na Ushirikishwaji Jumuishi, kuanzia Serikali Kuu, Sekta Binafsi, hadi Asasi za Maendeleo. Kupitia jukwaa hili, tunahimiza ushirikiano wa wadau wote wakuu wa mihimili ya uchumi, pamoja na Jumuiya ya Kimataifa na Mabalozi, kwa maslahi mapana ya Taifa.

Tunaamini kuwa Unicorn Allianz State Summit itakuwa chachu ya maendeleo ya Taifa, ikijenga Tanzania yenye Dira ya Pamoja, Sauti Moja, na Mshikamano Imara, inayounga mkono kikamilifu jitihada za Serikali na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Tunatoa wito kwa wawekezaji, mashirika ya umma, sekta binafsi, NGOs, mashirika ya maendeleo, pamoja na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) kuunga mkono jitihada hii ya kihistoria kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.

Dirisha la usajili sasa limefunguliwa, na washiriki wanahimizwa kufanya usajili mapema kupitia tovuti ya www.uaglobal.one kabla ya tarehe 30 Desemba 2025. Washiriki wote watahudhuria mkutano kupitia taasisi au makampuni wanayoyawakilisha, ili kuhakikisha ushiriki wa kimkakati, wenye tija na unaoendana na hadhi na ukubwa wa mkutano huu wa kihistoria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *