Akizungumza katika mahojiano maalum na UN News Kiswahili Frida amesema “Ni nafasi kubwa sana ambayo nimeipata. Sio kwangu tu, ni kwa ajili ya vijana wenzangu”.

Kilichomsukuma kupenda mazingira

Frida anasema changamoto alizokiona akiwa mdogo Arusha Tanzania zilimfanya kuwa msukumo wa kuhamasisha ulinzi wa mazingira. “Nilipata nafasi ya kusoma na kuona wasichana wawili waliolazimika kuhama Monduli kwa sababu ya ukame, njaa na umaskini. Ilinifanya nijisikie vibaya kuona wengine wanateseka. Nikatamani kuja kuwa mmoja wa watu wanaoweza kufanya jambo kwa ajili ya kuleta mabadiliko”.

Changamoto Kubwa: Utupaji wa taka za plastiki na Kudhoofisha Ikolojia

Akizungumzia changamoto za mazingira, Frida amebainisha hatari kubwa ni kutotambua athari za matendo yetu “Kama unakata mti bila kujua, au ukitupa taka  za plastiki popote pale, kuna madhara makubwa kwa dunia. Tunapoteza viumbe hai na tunadhoofisha ikolojia yetu.”

Ameeleza njia ya suluhisho kuwa “Wakati ni sasa tutafute namna ya kuachana na plastiki, kupunguza matumizi na kudhibiti taka kutoka viwandani na  kwa jumla.”

Sheria zinafaa lakini zisimamiwe

Frida amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa sera akihoji  “Tuna sera nzuri, lakini watu wangapi wanazisimamia? Tunahitaji kuongeza nguvu katika usimamizi wa sera hizi ili zifanye kazi kweli.”

Akizungumzia mafanikio yake akiwa kijana, Frida amesema, “Siri yangu kubwa ni Mwenyezi Mungu, pili ni kutokukata tamaa na kuamini katika ndoto zangu. Nilikua na ndoto ya kufanya mabadiliko duniani, na nimeendelea kusimama nyuma yake.”

Frida Amani (kulia), msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kwa hip hop au muziki wa kufokafoka almaarufu kama rap kutoka nchini Tanzania, ambaye pia ni mwanamazingira wa UNEP.

Frida Amani (kulia), msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kwa hip hop au muziki wa kufokafoka almaarufu kama rap kutoka nchini Tanzania, ambaye pia ni mwanamazingira wa UNEP.

Kuiga wengine na kuongeza mchango wa vijana

Frida anawaongoza vijana wengine kwa mfano “Ninaona vijana wengi wanafanya mambo makubwa duniani. Kwa upande wa mazingira, nimemuona binti mdogo wa Kitanzania, Lauren Kivuyo, akiendesha juhudi za kutunza miti na mazingira kwa ujumla.”

Frida amesema kuwa ndoto zake nyingi zinazohusiana na mazingira zinamfanya kushughulika usiku na mchana na wakati mwingine kumkosesha hata usingizi “Naogopa siku moja tuwe tumekaa hapa bila kuzitimiza ndoto zetu. Kazi ni nyingi na unapaswa kupambana sana kufanikisha ndoto hizo.”

Anewataka vijana wenzake kujishughulisha na kujifunza kutoka kwa wengine hasa linapokuja suala la mazigira na kurejesha ikolojia akiamini  kwamba kila mtu na kila kijana anawajibu na mchango katika kurejesha ikolojia.Top of Form

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *