Rombo. Zaidi ya wanariadha na wakimbiaji 3,000 wanatarajiwa kushiriki mbio za Rombo Marathon zitakazofanyika Desemba 23, 2025 katika Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza michezo, utalii wa ndani na uhifadhi wa mazingira.

Mbio hizo, ambazo zinafanyika kwa mara ya nne, zitakwenda sambamba na matukio ya kijamii yakiwemo nyama choma festival, matembezi na kukimbia msituni, pamoja na burudani za vyakula vya asili kama ng’ande, ngararimo na kinywaji cha asili cha mbege. Waandaaji wamesema tukio hilo limepangwa kuwa zaidi ya mashindano ya mbio, bali jukwaa la burudani na mapumziko kwa familia na wageni wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema Rombo Marathon ya mwaka huu itakuwa ya kipekee kwa kuwa itachukua siku tatu, ikijumuisha mbio na Ndafu Festival.

Mbio hizo zitafanyika katika msitu wa Rongai, eneo linalotoa mandhari ya kipekee ya Mlima Kilimanjaro, mito na mazingira ya asili yanayovutia wakimbiaji na watalii.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala akitoka katika moja ya hema (tenti) lililoandaliwa kwa ajili ya washiriki wa mbio za Rombo Marathon zitakazofanyika Desemba 22, kuelekea siku ya tukio Desemba 23. Picha na Janeth Joseph

“Rombo Marathon si mbio za siku moja. Ni tukio la siku tatu lenye mbio, burudani na mapumziko. Mshiriki anawasili Desemba 22 kwa mapumziko, Desemba 23 anakimbia na kufurahia burudani, huku akishuhudia uzuri wa mazingira ya Rombo,” amesema Mwangwala.

Ameongeza kuwa tukio hilo si kwa Wachaga pekee bali kwa Watanzania wote na wageni wanaotaka kupumzika wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Amesema wilaya imeandaa malazi ya makundi mbalimbali ikiwemo ya kawaida na ya wageni maalumu (VIP), huku usalama ukiwa umeimarishwa.

“Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, tumejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wageni wote kuanzia kuwasili hadi kuondoka,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwangwala amesema Desemba 24, 2025 wilaya imepanga kupanda miti zaidi ya 10,000 kama sehemu ya mkakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamati ya Maandalizi ya Rombo Marathon, Joseph Katembo amesema usajili unaendelea vizuri na zawadi zimeandaliwa kwa washindi wa makundi mbalimbali ya mbio. Alisema washiriki wa kilomita 21, 10 na tano watapata zawadi kulingana na nafasi zao, huku lengo likiwa kuhamasisha ushiriki mkubwa zaidi.

“Ninawaomba Watanzania wajitokeze kushiriki Rombo Marathon, maana ni mbio zitakazoiweka Rombo kwenye ramani ya michezo na utalii,” amesema Katembo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *