
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh19.9 milioni kwa Taasisi ya Moyo ya Hospitali ya Muhimbili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono sekta ya afya na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akikabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Benki ya Stanbic Mkoa wa Dar es Salaam, Edditrice Marco alisema msaada huo umetolewa kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSI), sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu benki hiyo kuanza kutoa huduma nchini.
Alisema benki inatambua mchango wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii, hivyo itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wagonjwa na watoa huduma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Hospitali ya Muhimbili, Dk Tatizo Waane ameishukuru Benki ya Stanbic kwa msaada huo, akisema vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuboresha huduma za tiba ya moyo.
Pia, ametoa wito kwa mashirika binafsi na wadau wengine kuendelea kushirikiana na sekta ya afya ili kuboresha huduma kwa Watanzania.