Kwa zaidi ya miaka kumi, shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limekuwa mshirika muhimu wa Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya nchini. Kupitia ushirikiano huu, THPS imechangia upatikanaji wa huduma za VVU, kifua kikuu, magonjwa ya mlipuko na yasiyoambukiza, pamoja na huduma nyingine muhimu za afya kwa mamilioni ya Watanzania.

Licha ya changamoto za rasilmali, ikiwemo kupungua kwa ufadhili katika sekta ya afya, unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU, umaskini, pamoja na ongezeko la maambukizi mapya hasa kwa vijana, THPS imeendelea kusimama imara. THPS inaamini kuwa kwa ushirikiano wa dhati, ubunifu na ushiriki wa jamii, maendeleo si ndoto tu bali ni jambo linalowezekana na linaloonekana kila siku.

Ushirikiano Unaoboresha Mwitikio wa Taifa Dhidi ya VVU

Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), THPS inaendelea kuimarisha huduma za kinga, matunzo na tiba ya VVU kote nchini.

Mkurugenzi wa Miradi wa CDC Tanzania, Dk George Mgomella.

Kupitia mradi wa Afya Hatua, THPS inashirikiana na vituo vya afya 364 katika mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga. Mradi huu umejenga uwezo wa wahudumu wa afya 1,176 na kuanzisha mifumo ya kidijitali inayoboresha utoaji wa huduma, uwajibikaji na matumizi ya takwimu.

Hadi sasa, zaidi ya watu milioni 3.1 wamepimwa VVU kupitia mradi wa Afya Hatua, huku wapokea huduma 192,731 wakianzishiwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huu, Dk. George Mgomella, Mkurugenzi wa Miradi wa CDC Tanzania, anasema:

“Kupitia ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau, tunaimarisha mwitikio wa VVU unaozingatia matokeo, uwajibikaji na manufaa ya pamoja.”

Kusogeza Huduma za Tiba Karibu na Jamii

Moja ya mafanikio makubwa ya THPS ni kusogeza huduma za VVU karibu na wananchi. Kupitia huduma mkoba, zaidi ya wapokea huduma 5,026 wanapatiwa dawa za kufubaza virisi vya UKIMWI katika maeneo yao, hivyo kuondoa safari ndefu na gharama za usafiri.

Katika kijiji cha Tandala mkoani Kigoma, huduma hii imeleta mabadiliko makubwa. Joshua Zengo anasema:

“Zamani nilikuwa natumia shilingi 12,000 kusafiri zaidi ya kilomita 50 kwenda Uvinza. Sasa huduma zinatufikia hapa kijijini. Afya yangu imeimarika, virusi vimefubaa, na nina muda wakutosha wa kufanya kazi za kilimo na kuitunza familia.”

Faida hizi zinaonekana kote nchini, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ufuasi wa tiba na matunzo, kupungua kwa msongo wa mawazo na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.

Zana za Kisasa za Uchunguzi wa VVU na Kifua Kikuu

Uchunguzi wa afya wa mapema huokoa maisha. THPS imesaidia kufunga mashine 73 za kisasa za uchunguzi wa Kifua Kikuu, zikiwemo mashine 18 za TrueNat na 55 za GeneXpert; machine hizi zinasaidia huduma katika mtandao wa  vituo vya afya 364 zikiwemo hospitali na zahanati. Vituo vyote hivi vimewezeshwa kuwa  na mifumo ya umeme wa akiba kwa nisahti ya jua.

Teknolojia hizi zimepunguza muda wa kusubiri majibu, zimewezesha kuanza matibabu mapema na kuboresha huduma, hasa vijijini.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nindo, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk Daniel Singolile.

Wahudumu wa afya wanasema hatua hii imeongeza ugunduzi wa mapema wa Kifua Kikuu na kulinda watu wanaoishi na VVU dhidi ya madhara makubwa ya kiafya.

Kuwezesha Wasichana na Kina Mama

Wasichana na kina mama bado wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya VVU kutokana na sababu za kibaiolojia, kiuchumi na kitamaduni. THPS inakabiliana na changamoto hii kupitia waelimishaji rika—wasichana vijana waliopata mafunzo wanaowafikia wenzao kwa elimu, ushauri na kuwaunganisha na huduma rafiki.

Kupitia mbinu hii, wasichana na kina mama 73,763 wamepata huduma za kinga dhidi ya VVU, ikiwemo matumizi ya dawa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.  Waelimishaji rika husaidia kupunguza unyanyapaa, kujenga kujiamini na kuwaunganisha vijana na huduma sahihi.

Huduma Jumuishi za VVU na Kifua Kikuu

THPS imewezesha vituo vya afya kutoa huduma za VVU na Kifua Kikuu sehemu moja. Mbinu hii huokoa muda, hupunguza unyanyapaa, huboresha ufuatiliaji wa wagonjwa na kuhakikisha matibabu yanaanza kwa wakati. Jamii zinathamini huduma hizi kwa kuwa ni rahisi, za heshima na zenye kuaminika.

Ubunifu wa Kidijitali na Nishati Endelevu

Mifumo ya kidijitali ni nguzo muhimu ya huduma bora. THPS imesaidia kuimarisha mifumo ya takwimu, usajili wa vidole na ufuatiliaji wa wapokea huduma katika vituo vya afya 364. Pia, mifumo ya nishati ya jua na umeme wa akiba imefungwa katika vituo hivyo.

Dk. Daniel Singolile, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Nindo, anasema:

“Kutokana na uwepo wa umeme wa akiba, mifumo yetu inaendelea kufanya kazi bila usumbufu. Huduma sasa ni za uhakika zaidi.”

Jamii Zinapoongoza, Mabadiliko Hutokea

Kupitia mradi wa Afya Hatua, THPS imeajiri wahamasishaji wa jamii 470, wakiwemo waelimishaji rika, mama walezi na vinara wa jamii. Kwa pamoja, wanasaidia kina mama 86,552 kuzingatia tiba, kuhudhuria kliniki, kufuatilia watoto wachanga na kupunguza unyanyapaa.

Muelimishaji rika Geresia Adriano kutoka Kasulu anasema:

“Kuwasaidia kina mama kujifungua watoto wasio na VVU ni kazi ninayojivunia. Inawaletea afya, matumaini na heshima.”

Huduma kwa Watu Wanaotumia Dawa za Kulevya

THPS pia inawezesha utolewaji wa  huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT) katika mikoa ya Pwani na Tanga. Zaidi ya watu 1,250 wamenufaika kwa kurejesha afya zao, kuacha uraibu na kurejea katika maisha ya kawaida.

Mzamilu Amiri kutoka Tanga anasema:

“Huduma ya MAT imenirejeshea afya, mahusiano na heshima. Kupona katika madhara ya uraibu kunawezekana.”

Kukabiliana na Ukatili na Kuimarisha Mifumo ya Afya

THPS imeunganisha huduma za VVU na mapambano dhidi ya ukatili, hasa kwa wanawake na watoto. Hadi sasa, wanusurika 170,367 wamepata msaada wa ulinzi, ushauri nasaha na rufaa.

Kwa kushirikiana na timu za afya za mikoa na halmashauri, THPS pia imechangia kuboresha mifumo ya afya, matumizi ya takwimu na ufanisi wa huduma. Mwaka 2024, THPS iliongoza Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana (VACS 2024), ambao matokeo yake yanaelezea ukubwa wa ukatili na namna unavyowaweka Watoto na vijana katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

Kusonga Mbele kwa Pamoja Katikati ya Misukosuko

Wakati misukosuko ya kimataifa na kitaifa ikiendelea kuathiri mifumo ya afya, THPS inaendelea kusimama imara ili kuhakikisha jamii zinaendelea kupata huduma za afya bora. Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dk. Redempta Mbatia, anasema:

“Changamoto kama mabadiliko ya ufadhili, vikwazo vya kijamii na mapungufu ya mifumo, zinatuchochea kubuni zaidi na kuimarisha ushirikiano. Tutaendelea kutoa huduma za VVU zilizo imara na zenye matokeo.”

Mshiriki wa programu ya MAT kutoka Tanga, Mzamilu Amiri.

Kupitia uwekezaji wa PEPFAR wa zaidi ya miaka 20 na ushirikiano wa Serikali, wadau na jamii, kwa pamoja, tunajenga taifa lenye afya njema—ambapo kila mtu ana nafasi ya kuishi maisha yenye utu, matumaini na bila VVU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *