Shambulio hilo lilitokea Jumanne jioni wakati wa swala, likilenga mahali pa ibada palipokuwa na waumini wengi na kuongeza orodha ya mashambulio ya kikatili yanayowalenga raia katika eneo hilo linalokumbwa na mgogoro.

Mratibu Mkazi na wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria, Mohamed Fall, amesema amehuzunishwa sana na taarifa za kupoteza maisha, akilielezea tukio hilo kuwa ni “shambulio la kinyama dhidi ya raia wasio na hatia.”

“Shambulio hilo, lililotokea wakati wa swala za jioni, lilisababisha kupotea kwa maisha na kuwaacha wengi wakiwa wamejeruhiwa,” amesema katika taarifa iliyotolewa Abuja.

Kwa mujibu wa duru za habari waumini watano wameuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Lawama na rambirambi

Katika taarifa yake iliyotolewa Maiduguri Bwana. Fall amejiunga na Gavana wa Jimbo la Borno, Profesa Babagana Umara Zulum, kulaani vikali shambulio hilo, akisisitiza kuwa maeneo ya ibada hayapaswi kamwe kulengwa.

“Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa nchini Nigeria, ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa familia za waliopoteza maisha, na kwa serikali na wananchi wa Jimbo la Borno,” amesema, huku akiwatakia majeruhi “afuweni ya haraka.”

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa pia amerudia wito wa gavana wa kuongeza umakini na kuimarisha hatua za usalama, hususan katika kipindi hiki cha sikukuu. “Huu ni wakati ambao jamii zinapaswa kukusanyika kwa amani, si kwa hofu,” ameongeza.

Mfululizo wa mashambulio ya mauaji

Shambulio la Soko la Gamboru ni la hivi karibuni katika msururu wa mashambulizi ya mauaji yaliyolikumba Jimbo la Borno mwaka huu.

Bwana. Fall amesema tukio hilo ni “ukumbusho mwingine wa kutisha wa gharama kubwa ya mashambulio ya kikatili katika Jimbo la Borno,” akirejelea shambulio la tarehe 5 Septemba huko Darajamal, katika eneo la Serikali ya Mtaa ya Bama, ambapo zaidi ya raia 50 waliuawa na wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi lenye silaha lisilo la kiserikali.

Mashambulio mengine yamehusisha kulengwa kwa jamii za vijijini na kambi za wakimbizi wa ndani, mara nyingi yakitumia vilipuzi vya kutengenezwa kienyeji na mashambulio ya kujitoa muhanga.

Wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na wasafiri wamekuwa wakilengwa mara kwa mara, hali inayozidisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Wito wa kulinda raia

Akisisitiza msimamo wa Umoja wa Mataifa, Bwana. Fall amewahimiza wahusika wote katika mgogoro huo kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. “Narudia wito wangu kwa pande zote katika mgogoro kulinda raia, wakiwemo wale waliokusanyika katika maeneo ya ibada, pamoja na mali zao, na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu,” amesema.

Licha ya changamoto za kiusalama zinazoendelea, Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa utaendelea kusimama na jamii zilizoathiriwa.

“Ili kukamilisha juhudi za Serikali, Umoja wa Mataifa unathibitisha upya dhamira yake ya kuendelea kusaidia watu walioathiriwa na mgogoro kaskazini-mashariki mwa Nigeria,” amesema Bwana. Fall, akisisitiza umuhimu wa msaada wa kibinadamu unaoendelea na ulinzi wa raia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *