Tarime. Baadhi ya wazee hao wamesema vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu zinapaswa kutumiwa kama funzo ili kuepuka hali kama hiyo kutokea huku wakitoa wito kwa wazee nchini kutimiza wajibu wao kama washauri na walezi wakuu wa jamii.
Wamesema matukio yaliyotokea ni kielelezo sahihi na halisi cha vita kwa maelezo kuwa vita haina macho ambapo madhara yake yanaikumba jamii nzima huku wakieleza kuwa wapo watu waliodhurika ingawa hawakuwa sehemu ya wale walioandamana.
Wazee hao wameyasema hayo Jumatano Desemba 24, 2025 wilayani Tarime mkoani Mara kwenye kimao kati yao na na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyasaho.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la KujengaTaifa, Rhimo Nyasaho akizungumza na baadhi ya wazee wa mkoa wa Mara wilayani Tarime. Picha na Beldina Nyakeke
Wamesema hawataki kusikia tena yaliyotokea wakati huo yakijirudia kwani madhara yake ni makubwa kisaikolojia na kiuhalisia sambamba na kiuchumi na kijamii pia.
“Tulikuwa kwenye wakati mgumu sana kujifungia ndani huku ukisikia milio ya risasi na mabomu na mbaya zaidi waliokuwepo na wasiokuwepo walipata madhara na hii ndio tafsiri ya vita,hili jambo tulikatae kwa nguvu zetu zote,” amesema Mugesi Daniel Mshauri kutoka Butiama
Ongati Msangya kutoka Rorya amesema wazee wanapaswa kutumiza wajibu wao wa malezi katika jamii na kamwe wasikubali yaliyotokea yakajirudia tena.
Amesema wazee wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi huku akitolea mfano namna ambavyo Rais wa awamu ya kwanza, hayati Mwl Julius Nyerere pamoja na mambo mengine aliwashirikisha wazee katika harakati za kudai uhuru wa nchi.
“Wazee tutafakari na kuchukua hatua,tuongee na vijana,tuwaelekeze kile wanapaswa kufanya kwani tukiwaacha mambo yataharibika,tuchukue hatua kulingana na mila na desturi zetu,amani ya nchi yetu ni bora kuliko kitu kingine,” amesema
Baadhi ya wazee wa mkoa wa Mara wakiwa kwenye kikao wilayani Tarime na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la KujengaTaifa, Rhimo Nyasaho. Picha na Beldina Nyakeke
Samson Marwa kutoka Wilaya ya Serengeti amesema wakati wazee wanashughulika na suala la malezi ya jamii hususan vijana, Serikali lia inapaswa kuangalia namna ya kuwawezesha vijana kuwa na shughuli za uhakika za kufanya ili kuwa na vyanzo vya kujipatia kipato.
“Kama vijana hawana namna nzuri ya kujipatia kipato ni rahisi sana mtu kuwarubuni na kufanya yale yasiyofaa lakini kama wana uhakika wa kipato haiwezekani wakarubuniwa,” amesema
Akizungumza na wazee hao,Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi amewashukuru wazee mkoani humo kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali hali ambayo imesaidia kuimarisha hali ya amani na utulivu ndani ya mkoa.
Amesema amani ikitetereka wanaopata shida ni wazee,akinamama na watoto hivyo wazee hao wanapswa kuendelea kuungana na Serikali ili kutokuruhusu
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyasaho amewashukuru wazee mkoani Mara kwa namna walivyoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha amani mkoani humo inaendelea kuwepo.
Amewataka wazee hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali jambo ambalo litasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
“Mkoa wetu bado uko nyuma kimaendeleo hata ukiangalia mji wa Musoma ambao ni makao makuu ya mkoa bado haujachangamka, sasa Serikali ina mipango mingi kwaajili ha kuchechemua uchumi wa mkoa na mipango hiyo itafanikishwa endapo kutakuwa na amani,” amesema
Amesema baadhi mipango iliyowekwa na Serikali kwaajili ya kuchochea uchumi wa mkoa na watu wake ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Musoma, reli ya Tanga Musoma na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwepo barabara za mkoa na zinazounganisha mkoa huo na mikoa ya jirani.
“Tunatakiwa kuidai Serikali maendeleo na hatuwezi kuidai maendeleo kama hakuna amani,wazee wangu nyie mna mchango mkubwa sana katika kusimamia amani ya nchi hii,niwaombe mfanye hivyo kisha tuanze kuidai Serikali maendeleo,”