
Dar es Salaam. Sh10 milioni zimetolewa kwa ajili ya kuwadhamini wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hatua inayolenga kuimarisha elimu na uhusiano wa kielimu kati ya Tanzania na China.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa udhamini huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu anayesimamia Taaluma, Profesa Baraka Maiseli, amesema ufadhili huo umetokana na mchango wa Shilingi milioni 10 uliotolewa na kampuni ya JUYE kwa lengo la kusaidia wanafunzi wanaojifunza lugha ya Kichina.
Profesa Maiseli amesema kuanzishwa kwa udhamini huo ni hatua muhimu katika kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kichina pamoja na ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na China.
“Natoa pongezi kwa JUYE pamoja na Taasisi ya Confucius kwa kuanzisha udhamini huu ambao utaongeza motisha kwa wanafunzi na kuimarisha mahusiano ya kielimu kati ya nchi zetu,” amesema Profesa Maiseli.
Aidha, amewapongeza walimu wa Kitanzania na Wachina wa Taasisi ya Confucius kwa mchango wao katika kukuza elimu na maendeleo ya vijana.
Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013, Taasisi ya Confucius katika UDSM imekuwa daraja muhimu la mawasiliano ya kielimu na kitamaduni kati ya Tanzania na China, ambapo kwa zaidi ya muongo mmoja imewahudumia wanafunzi zaidi ya 60,000 wa Kitanzania sambamba na kuendesha shughuli za utamaduni na programu za kubadilishana uzoefu.
Kwa mujibu wa Profesa Maiseli, jitihada hizo zimezalisha wataalamu wengi wenye uelewa wa lugha ya Kichina na mtazamo wa kimataifa, ambao kwa sasa wanachangia maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, elimu na utamaduni.
Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius upande wa Tanzania, Dk Mussa Hans, amesema ufadhili huo ni ishara ya kutambua juhudi za wanafunzi waliofanya vizuri na kuwahamasisha kuendelea na hatua inayofuata ya masomo yao.
“Elimu ni daraja linalovuka mipaka ya kitaifa. Ufadhili huu hautawapunguzia tu wanafunzi mzigo wa ada katika ngazi inayofuata, bali utaendelea kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na kielimu kati ya China na Tanzania,” amesema Dk Hans.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya JUYE Tanzania, Xu Hongjuan, amesema udhamini huo unalenga kuwatambua na kuwahamasisha wanafunzi wanaojifunza lugha ya Kichina, akisisitiza kuwa lugha hiyo ni nyenzo muhimu ya kuunganisha tamaduni na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Amesema maendeleo makubwa yanayoonekana kwa wanafunzi, kutoka hatua ya kuogopa kuzungumza hadi kuweza kuzungumza kwa ufasaha na kusoma mashairi ya Kichina, ni ushahidi wa bidii na dhamira yao.
Xu ameahidi kuwa JUYE itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu nchini ili kuchangia maendeleo ya vijana na kuhimiza wanafunzi kuwa mabalozi wa ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo imeshiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Daraja la Mwanza (Magufuli), Uwanja wa Samia Arusha, Daraja la Tanzanite, Daraja la Juu la Ubungo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dodoma, bandari za Dar es Salaam na Tanga, pamoja na miradi ya BRT, Reli ya Kisasa (SGR) na miradi ya maji jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wanufaika wa udhamini huo, Muhsin Abubakar Juma, amesema kujifunza lugha ya Kichina ilikuwa ndoto yake ya muda mrefu, akiamini itamsaidia katika shughuli zake za kibiashara nchini China.
Naye Zuhura Hassan amesema kupitia udhamini huo amepata punguzo la asilimia 70 ya ada, huku akiwashauri vijana kujifunza lugha ya Kichina kutokana na kuongezeka kwa viwanda na biashara kati ya Tanzania na China, hali itakayowarahisishia kupata ajira.