Hatua hii imetangazwa leo huko Dakar nchini Senegal. Hatua za WFP, zinazotekelezwa katika Burkina Faso, Cameroon, Chad, Côte d’Ivoire, Mali, Mauritania, Niger na Nigeria, zimelenga jamii zinazokabiliwa na hali mbaya zaidi ya kutokuwa na uhakika wa chakula zikiwemo zile zilizoathiriwa na migogoro, majanga ya asili na uhamishaji wa kulazimishwa.
Msaada huo unaofadhiliwa na EU umekuja katika kipindi ambacho ufadhili wa kibinadamu umekuwa ukipungua kwa kiasi kikubwa, huku takribani watu milioni 52 sawa na karibu asilimia 12 ya wakazi wa eneo hilo wakitarajiwa kukumbwa na njaa kali katika msimu wa wa Juni hadi Agosti.
Wakimbizi wengi wakiwa wanawake na watoto waliokimbia machafuko El-Fasher
WFP na wadau wanafanya kila liwezekanalo
Licha ya changamoto kubwa za ufikiaji na usafirishaji katika eneo hilo, WFP na wadau wake wameonesha wepesi wa kiutendaji na dhamira thabiti kwa kuwafikia watu milioni 3.3 kupitia mchanganyiko wa msaada wa fedha taslimu na ugawaji wa chakula, pamoja na msaada maalum wa lishe kwa watoto walio chini ya umri wa miaka miwili.
Nchini Burkina Faso pekee, zaidi ya watu 221,000 wakiwemo watu 124,800 wakimbizi wa ndani ya nchi (IDPs), wamepokea msaada muhimu wa chakula. Hatua hii imesaidia asilimia 86 ya familia kuepuka mikakati ya hatari ya kukabiliana na njaa kama kuruka milo, kuuza mali muhimu au kuwaondoa watoto shuleni.
Matokeo yake, asilimia 60 ya familia zimefikia viwango vinavyokubalika vya matumizi ya chakula, kutoka asilimia 13 pekee kabla ya mwitikio wa WFP mwezi Juni 2025.
Nchini Cameroon, ufadhili wa EU umekuwa muhimu, ambapo hatua mahsusi za msimu wa kutokuwa na uhakika wa chakula zimewafikia watu 58,700 asilimia 57 kati yao wakiwa wanawake kupitia msaada wa fedha taslimu na tani metri 159 za vyakula. Msaada huo wa fedha haukujibu tu mahitaji ya dharura ya chakula bali pia umechochea masoko ya ndani na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
Katika nchi za Chad, Côte d’Ivoire, Mali, Mauritania, Niger na Nigeria, hatua za haraka na zenye kubadilika za WFP zimetoa nafuu ya haraka kwa wakimbizi, waliorejea, jamii zinazowahifadhi wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makazi yao hivi karibuni, mara nyingi zikifikisha chakula ndani ya saa 72 tangu uhamishaji.
Wasicha wakisoma pamoja shuleni nchini Senegal
Njaa ambayo haijawahi kushuhudiwa
Mkurugenzi wa Kanda wa WFP kwa Afrika Magharibi na Kati, Margot van der Velden, amesema kuwa kiwango cha njaa katika eneo hilo mwaka huu hakijawahi kushuhudiwa, na kwamba kwa msaada thabiti wa EU na wadau, WFP imeweza kuwafikia mamilioni ya watu waliokuwa ukingoni mwa njaa kali, ikitoa si chakula pekee bali pia matumaini na uthabiti kwa jamii zilizo katika mgogoro.
Ameongeza kuwa dhamira ya EU ni nguzo muhimu katika uwezo wa WFP wa kuchukua hatua haraka na kwa ufanisi katika moja ya mazingira magumu zaidi ya kibinadamu duniani.
Ukosefu wa chakula na utapiamlo Afrika Magharibi na Kati unasababishwa hasa na migogoro, watu kufurushwa makwao, hali mbaya ya hewa, kuyumba kwa uchumi na bei ya juu ya vyakula.
Sababu hizi zinadhoofisha uwezo wa watu kujilisha imesema WFP. Watu waliolazimika kuhama makazi yao wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa njaa kali baada ya kukatwa kutoka mashamba na maeneo yao ya malisho.
Zaidi ya watu milioni 11 wamelazimishwa kuhama katika eneo hilo, wakiwemo wakimbizi na wanaotafuta hifadhi milioni 3.1, na watu milioni 8.2 waliokimbia makazi yao ndani ya nchi katika Sahel ya kati, Bonde la Ziwa Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
EU ni mmoja wa wadau wa muda mrefu wa WFP, ikisaidia si tu kukabiliana na migogoro ya chakula na lishe bali pia kuunga mkono uchambuzi wa kijiografia wa usalama wa chakula wa WFP katika eneo hilo, kwa kutoa takwimu za wakati, zenye ufanisi wa gharama na za kuaminika kwa mifumo ya tahadhari ya mapema, tathmini za uhatari na ulengaji wa afua za kibinadamu na maendeleo.
WFP inatoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya kibinadamu na kupanua suluhisho endelevu, ikisisitiza kuwa mkabala huo ni muhimu katika kupunguza utegemezi wa muda mrefu wa misaada ya dharura.