KAMA wewe ni shabiki wa Yanga utakumbuka kwamba miongoni mwa sajili zilizotikisa ulikuwa wa kiungo mshambuliaji ni Andy Boyeli, Lakini cha kushangaza ni kwamba klabu hiyo imembwaga kimyakimya.

Boyeli ambaye alitua Yanga kwa mkopo akitokea Sekhukhune ya Sauzi, amecheza miezi sita akiweka rekodi ya kufunga mabao mawili katika mechi tano alizopata nafasi ya kucheza.

Iko hivi, mabosi wa Yanga walimsajili mshambuliaji huyo kwa matarajio makubwa ya kwamba atakwenda kuisaidia timu hiyo hasa eneo la mbele baada ya kuondoka kwa Muivory Coast Stephane Aziz KI.

Lakini mambo yalibadilika baada ya msimu kuanza kwani kiungo huyo hakuweza kutoboa kwenye hesabu za kocha kijana Romain Folz ambaye alianza kukinoa kikosi hicho mwanzoni kabisa.

Baada ya kuondoka Folz alitua Pedro Goncalves ambaye alianza kazi mwezi Oktoba, lakini nako Boyeli hakuweza kupenya kwenye kikosi cha kwanza, huku akipata nafasi akitokea benchi muda mwingi.

RIPOTI YA KOCHA YAMNG’OA

Unaambiwa Pedro alipowapatia mabosi wa klabu hiyo ripoti ya awali, moja kati ya maeneo ambayo alitaka kuongezewa nguvu ni mbele hasa kiungo na mshambuliaji.

Taarifa za ndani ya Yanga zimedai kuwa, “kocha amehitaji nguvu maeneo hayo kwa sababu Clement Mzize yuko nje kwa majeraha na Dube ndiye aliyesalia.

“Kiwango cha Boyeli hakijamridhisha ndio maana hamuamini sana kumuanzisha kikosi cha kwanza, hivyo amehitaji aongezewe nguvu hasa kuelekea michuano ya kimataifa.”

MIPANGO IKO HIVI

Kwa sasa mabosi wa Yanga wanasaka kiungo mshambuliaji ambaye atakwenda kurithi nafasi ya Boyeli, lakini asiwe ameshiriki michuano ya CAF msimu huu ili aweze kucheza.

Mwanaspoti liliwahi kuandika kuwa Yanga imemtuma legendari aliyekuwa akikipiga katika kikosi hicho, Khalid Aucho, kuzungumza na Okello ambapo kiungo huyo wa zamani anaeheshimika kwa mastaa wote wa Taifa hilo.

Lakini Okello bado ana mkataba mrefu na Vipers ambayo bosi wao ni mtata kuuza mastaa wake wakubwa akiwemo kiungo huyo ambaye ni nahodha wa timu hiyo.

Simba iliwahi kumtaka Okello huko nyuma lakini licha ya kufanya majaribio mawili ya kumsajili mchakato huo ulikwamia kwa viongozi wa Vipers. Hata hivyo amecheza hatua ya awali ya michuano ya CAF mpaka hapo yuko nje ya mahitaji ya Yanga kimataifa.

Jina lingine ambalo Yanga inapambana nalo ni kiungo mwingine ni Kikwama Mujinga ambaye naye ni nahodha huko anakoitumikia klabu yake ya Reneissance ya kwao DR Congo.

Mujinga ni staa muhimu wa Reneissance ambayo tayari imeshapokea ofa lakini inaweka ngumu kumuachia kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi chao.

Katika kufanyia kazi pendekezo la kocha Pedro la kutaka kuletewa straika mpya anayejua kufunga mabao, mabosi wa Yanga wamehamia kwa nyota wa timu ya taifa ya Angola, Gelson Dala anayekipiga kwa sasa katika klabu ya Al-Wakrah ya Qatar, ili kama mambo yataenda sawa jamaa atue dirisha dogo kuitumikia timu hiyo ya Jangwani.

Yanga inaendelea kujifua kwa mazoezi makali kambini, huku ikijiandaa kufunga safari kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *