
Morogoro. Watu 10 wamefariki dunia huku wengine 18 wakijeruhiwa katika ajali barabarani iliyohusisha basi la abiria aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bill Mawio, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo aina ya Howo lenye tela, mali ya Kampuni ya Kikori. Magari yote mawili yaliteketea kwa moto baada ya ajali hiyo.
Ajali hiyo imetokea jioni ya Desemba 31, 2025, katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam. Basi la abiria lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Swalehe Adamzi, likitokea Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani Msamvu, Morogoro, kuelekea Mkoa wa Tanga, huku lori la mizigo likiwa na shehena ya mbolea likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro iliyotolewa kwa vyombo vya habari, waliofariki dunia ni abiria wa basi hilo, wakiwemo wanaume wanane na wanawake wawili. Majeruhi ni 18, wakiwemo wanaume tisa na wanawake tisa, ambapo watoto ni watano, kati yao wavulana watatu na wasichana wawili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori la mizigo aliyefahamika kwa jina moja la Abuu, mkazi wa Msoga, Chalinze mkoani Pwani, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 26 hadi 28. Inadaiwa dereva huyo alijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha na kusababisha barabara kuwa na utelezi.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro imethibitisha kupokea majeruhi pamoja na miili ya marehemu. Scholastika Solomon, Kaimu Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri huku wakiendelea kupatiwa matibabu ya kina, wakati shughuli ya utambuzi wa miili ya marehemu ikiendelea.
“Majeruhi hawa wamepokewa wakiwa na hali mbalimbali, wengine wanamivunjiko na michubuko katika maeneo mbalimbali ya miili yao, lakini mpaka sasa hivi madaktari wapo kazini na kila mmoja anahudumiwa kulingana na hali yake,” amesema Scholastika.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za haraka pindi ajali au majanga yanapotokea ili kusaidia uokoaji wa maisha na mali. Daniel Myala, Ofisa Operesheni wa jeshi hilo mkoani hapa, amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria za usalama wa barabarani.
“Mpaka tunafika eneo la tukio na kufanya maokozi watu 10 tayari wameshafariki majeruhi walikuwa 18 ambao tumewakimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi,” amesema Myala.
Samson Mmali, miongoni mwa majeruhi ameeleza kuwa licha ya dereva wa lori kuvamia njia yao, pia dereva wa basi walilokuwa wakisafiri alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi, hali iliyochangia ukubwa wa ajali hiyo.
“Ile ajali ilitokana na lori la mizigo lilikuwa linataka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila tahadhari na dereva wetu alikuwa kwenye mwendokasi kwa hiyo akashindwa kulimudu gari,” amedai Mmali.