Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa hotuba ya kufunga mwaka 2025 iliyolenga kujenga umoja wa kitaifa, wachambuzi wa siasa wametoa maoni tofauti, baadhi yao wakieleza kwamba azma yake ya kujenga umoja wa kitaifa imechelewa.

Jana, Jumatano Desemba 31, 2025, katika hotuba yake ya kufunga mwaka na kuukaribisha mwaka 2026, Rais Samia alisema Serikali imejipanga kujenga umoja wa kitaifa nchini huku akiwataka Watanzania wasikubali tofauti za kimtazamo ziwagawe.

Alibainisha kuwa katika kulifanikisha hilo, hatua za kuunda Tume ya maridhiano zimeanza kuchukuliwa na Serikali itashirikiana na wadau wote katika kukubaliana kuhusu muundo wa Tume, aina ya wajumbe, majukumu yao na muda wa kazi wa Tume hiyo.

Wachambuzi wa siasa wamekuwa na maoni mseto, wakisema hatua ya kujenga umoja wa kitaifa ilitakiwa kuanza muda mrefu na kuwa kabla ya kufikia ngazi hiyo, waliohusika na yaliyotokea Oktoba 29, wawajibike au wawajibishwe.

Hata hivyo, baadhi yao wamesema hotuba hiyo imelenga kuwaleta pamoja Watanzania kuishi katika utamaduni wa umoja na mshikamano kwa masilahi ya Taifa, jambo ambalo linahitajika kwa sasa kuliko wakati mwingine.

Oktoba 29, 2025 wakati wa uchaguzi kulitokea maandamano yaliyoambatana na vurugu zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa mali katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Songwe, Dodoma na Arusha.

Kufuatia matukio hayo, Novemba 18, 2025, Rais Samia aliunda Tume ya kuyachunguza ambayo inaendelea na kazi chini Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande.

Wachambuzi hao wa siasa wameeleza hayo leo Alhamisi Januari mosi, 2026 wakati wakitoa maoni yao kuhusu hotuba hiyo ya Rais Samia aliyoitoa, katika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.

Miongoni mwao, Dk Hezron Makundi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), amesema sehemu ya hotuba ya Rais Samia imebabeba dhamira ya usuluhishi, kwamba makundi yote nchini yatapewa fursa katika kushiriki mchakato wa kuleta umoja wa kitaifa.

“Lengo ni maridhiano ambayo ni ya makundi yote ya Taifa letu, kutakuwa na ujumuishi kwa maana kila kundi katika jamii litapewa fursa iwe kwa kushiriki moja kwa moja au kutoa mapendekezo,” ameeleza Dk Makundi.

Sambamba na hilo, Dk Makundi amesema hatua ya Rais Samia, kuja na juhudi hizo inapaswa kupongezwa na Watanzania wanatakiwa kuipokea kwa mikono miwili.

“Huyu (Rais Samia) ni kiongozi wa kitaifa, anayeiongoza nchi katika mwelekeo unaofanya, tuendelee kuwa na umoja. Hili linajikita katika historia ya Taifa ambayo kila siku tumekuwa kitu kimoja, lakini haizuii kutofautiana kisiasa na kiimani,” amesema Dk Makundi.

Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa siasa na uchumi, Gabriel Mwang’onda amesema hatua ya kuwepo kwa mchakato wa maridhiano ili kujenga Taifa ni jambo lisiloepukika na lilitarajiwa ili nchi isonge mbele.

“Inawezekana watu wakawa na mitizamo tofauti licha ya kwamba kuna mambo yaliyotokea Oktoba 29, lakini kuna Tume inayofanya uchambuzi kujua sababu za yale yaliyotokea,” amebainisha.

Mwang’onda amesema hatua zilizochukuliwa na Rais Samia kuhusu suala hilo, zinaonyesha dalili nzuri kwa Serikali na Watanzania kuongea lugha moja.

“Hapo awali wananchi ndio walikuwa wanasema tumepata madhila, tumepoteza ndugu zetu, lakini upande wa watawala ilikuwa tofauti kidogo na Watanzania. Sasa hivi taratibu tumeanza kuona kuna kauli zinaashiria kwamba tumepoteza ndugu zetu.

“Sasa kauli kama hizi zimeanza kufanya viongozi na raia kuongea lugha moja kwa sababu inakuwa mbaya pale ambapo wananchi wanakuwa na lugha yao na viongozi wana lugha yao,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Mwang’onda, ukiona lugha zinaanza kushabihana basi kuna nia thabiti inayolenga kuleta maridhiano miongoni mwa Watanzania.

“Ni hatua nzuri iliyochukuliwa na Rais Samia, japo kuna watu wanaweza wakasema, haina maana lakini msingi kinachoeleweka hatuwezi kurudisha uhai kwa ndugu zetu waliotutangulia.

“Kinachotakiwa kukifanya ni yaliyotokea yasijirudie, tunafanyaje yasijirudie ndio hizi hatua zilizoanza kuchukuliwa za Tume ya maridhiano kuundwa na ile Tume ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29,” amesema.

Mwang’onda amesema Tume hizo mbili ni za msingi, ingawa kuna madai yapo hasa ya kisiasa ikiwemo nani atakuwepo katika hiyo Tume, je, taasisi za kidini zitahusika au vyama vya siasa pekee na asasi za kiraia.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Aviti Mushi amesema kujenga umoja wa kitaifa ni jambo muhimu sana, ingawa mchakato huo umechelewa.

“Yaliyosababisha au yaliyotokea mwaka 2025, hayakuanza siku moja au mbili, mfano Oktoba 29 yalianza muda na nafasi ilikuwapo ya kujenga huu umoja.

“Siku za mwanzo, Rais Samia alikuja na 4R (maridhiano, kujenga upya, ustahimilivu na mageuzi), ilikuwa njia nzuri sana, lakini sijui ikawaaje zikaachwa, huenda ni miongoni mwa sababu za haya kutokea,” amesema Dk Mushi.

Dk Mushi amesema hivi sasa baadhi ya Watanzania wana uchungu mioyoni mwao na wanashindwa kuzungumza, kinachopaswa kufanyika ni Serikali kukiri kwamba kuna makosa yamefanyika na kuwaomba radhi wananchi.

“Ili kusonga mbele inatakiwa waliobainika kufanya makosa kuwajibika, kisha tujenge umoja wa kitaifa wa Watanzania kuponya maumivu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *