
Arusha. Chama cha Waendeshaji Watalii Tanzania (Tato) kimezitaka taasisi, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii nchini kuwekeza katika ujenzi na uwasilishaji wa simulizi zenye nguvu kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kimesema kwa kufanya hivyo kutaongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Januari Mosi, 2026 na Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo kwa wanachama na wadau wa sekta ya utalii.
Amesema ushindani wa sasa katika soko la utalii duniani haupimwi tena kwa bei nafuu au idadi ya wageni pekee, bali kwa uwezo wa nchi au eneo kujitambulisha kupitia hadithi halisi, zenye mvuto na maana kwa msafiri wa kisasa.
Kwa mujibu wa Chambulo, wasafiri wa leo hawaridhiki tena na kutazama mandhari nzuri peke yake, bali wanatafuta uzoefu unaogusa hisia, unaoonyesha uhalisia na kujenga muunganiko wa kweli kati yao na maeneo wanayotembelea.
“Katika muktadha huo, Tanzania ina utajiri mkubwa wa hadithi kuanzia wanyamapori wa kipekee, mandhari ya asili, tamaduni mbalimbali, hadi jitihada za uhifadhi na mchango wa jamii zinazozunguka maeneo ya utalii,” amesema.
Amesisitiza kuwa changamoto kubwa si ukosefu wa vivutio, bali namna vinavyowasilishwa kwa dunia.
Chambulo amesema mwaka huu mpya pia utumike kuwaelimisha wadau na wawekezaji wa utalii kuhusu mwelekeo wa sasa wa soko la kimataifa, ili Tanzania iweze kunufaika zaidi na ongezeko la watalii pamoja na mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Amesema matumizi ya lugha za jumla na matangazo yasiyo na mwelekeo mahsusi hayavutii tena, akisisitiza kuwa kila kivutio kinapaswa kusimuliwa kupitia hadithi inayoonyesha utu, thamani na uzoefu wa kipekee unaopatikana nchini.
“Mustakabali wa utalii unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya waendeshaji wa utalii, Serikali, jamii na washirika wa kimataifa, ili kuunda simulizi zenye nguvu zitakazoiweka Tanzania kama chaguo la makusudi kwa wasafiri wanaotafuta ubora badala ya wingi,” amesema Chambulo.
Ameongeza kuwa bila mshikamano na dira ya pamoja, wadau wataendelea kulaumiana badala ya kushiriki kikamilifu katika kufikia malengo ya taifa ya kukuza utalii.
Aidha, amesema mkakati wa kusimulia hadithi za vivutio utaenda sambamba na kujenga uhusiano wa muda mrefu na masoko teule, hususan washauri wa safari maalum na waendeshaji wa utalii wa niche, wanaotambua kwa kina thamani ya vivutio vya Tanzania.
“Njia hii inalenga kuvutia wageni wenye tija zaidi na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa,” amesema.
Hata hivyo, kauli hiyo inatolewa wakati Tanzania inakadiriwa kupokea zaidi ya watalii milioni tano kwa mwaka, huku Serikali ikiweka lengo la kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, mmoja wa wanachama wa Tato, Athumani Njiku ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Solo Adventure, amesema wameupokea ujumbe huo kwa uzito na wako tayari kuutekeleza kwa vitendo.
Amesema wadau wa sekta hiyo wamejipanga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarisha ushindani wake na kufanya vizuri zaidi katika soko la utalii duniani.