Serikali ya Cuba imetangaza kwamba raia wake 32 waliuawa wakati wa shambulio la Marekani dhidi ya Venezuela siku ya Jumamosi, ambapo askari wa kikosi maalumu wa Marekani walimteka nyara Rais Nicolas Maduro na mkewe na kuwapeleka New York.

Cuba imetangaza maombolezo ya siku mbili kwa raia wake waliouawa katika shambulio la Marekani, ikisema kwamba mipango ya mazishi itatangazwa baadaye.

Serikali ya Cuba imeeleza katika taarifa yake kwamba “wanajeshi waliouawa, wote wakiwa wanachama wa Jeshi la Mapinduzi au Wizara ya Mambo ya Ndani ya Cuba, walikuwa nchini Venezuela,” kwa ombi la serikali ya Caracas. Taarifa hiyo imeeleza kwamba Wacuba 32 waliuawa katika mapigano ya moja kwa moja na washambuliaji au kutokana na milipuko ya makombora.

Taarifa hiyo imesema, “Katika kutimiza majukumu yao ya usalama na ulinzi, raia wetu walitekeleza wajibu wao kwa heshima na ushujaa na waliuawa baada ya mapambano makali katika mapigano ya moja kwa moja dhidi ya washambuliaji au kutokana na mabomu yaliyolenga taasisi mbalimbali.”

Cuba na Venezuela zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, na mnamo 2002, jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais wa wakati huo wa Venezuela, Hugo Chavez liliihimiza Cuba kuingilia kati masuala ya kijeshi ya nchi hiyo ili kuimarisha mamlaka yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *