Burkina Faso ilikumbwa na hali ya wasiwasi siku za Jumamosi na Jumapili ya jana, kufuatia ripoti za kuwepo jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais wa mpito wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré.

Harakati za kijeshi na viwango vya juu vya tahadhari vimeshuhudiwa katika mji mkuu, Ouagadougou na jiji la Bobo-Dioulasso, huku vyombo vya usalama na vyombo vya habari vikiripoti kuimarishwa vikosi vya jeshi mbele ya kambi ya Baba-Sy, moja ya vituo maarufu zaidi vya kijeshi katika mji mkuu, jambo ambalo limetia nguvu madai ya kuwepo mgawanyiko ndani ya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

Serikali ya Burkina Faso haijatoa taarifa kamili rasmi kuhusu kilichotokea, lakini vyombo vya habari vya ndani na kimataifa vimesambaza taarifa zinazokinzana, huku ripoti zikizungumzia kamata kamata inayoendelea ndani ya jeshi. Baadhi ya maafisa wa jeshi pia wanatuhumiwa kuhusika katika “njama ya mapinduzi”.

Kwa upande mwingine, vyombo vya habari vilivyo karibu na serikali vimemtuhumu rais wa zamani wa Burkina Faso, Paul Henry Sandogo Damiba, ambaye anaishi uhamishoni nchini Togo, kuwa anahusika katika harakati za hivi karibuni.

Tuhuma hizi zinakuja katika muktadha wa mfululizo wa kesi na kukamatwa kwa wanajeshi wanaotuhumiwa kula njama dhidi ya utawala wa sasa tangu Septemba mwaka jana, zikionyesha mzozo unaoendelea kati ya makundi ya utawala wa zamani na wa sasa.

Sambamba na hayo, makundi ya kiraia yanavyounga mkono serikali, kama vile “Harakati ya Uamsho ya Wananchi ” yamejitokeza mitaani kumuunga mkono kiongozi wa sasa wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré.

Traore anakabiliwa na changamoto nying tangu alipoingia madarakani mnamo Septemba 2022 kupitia mapinduzi ya kijeshi, huku makundi yenye silaha huko kaskazini na mashariki mwa nchi yakiendelea kutishia usalama wa ndani. Vilevile majaribio ya mapinduzi ndani ya jeshi yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara, jambo linaloonyesha mzozo unaoendelewa kutokota ndani ya nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *