Jeshi la Sudan limetangaza leo Jumatatu kwamba limedungua ndege zisizo na rubani za waasi wa Rapid Support Forces (RSF) zilizojaribu kushambulia bwawa na makao makuu ya kambi mbili za kijeshi, huku vyanzo vya matibabu vikithibitisha kwamba watu 114 wameuawa katika wiki moja katika mashambulizi tofauti katika eneo la Darfur, huko magharibi mwa Sudan.

Ripoti zinasema kuwa mizinga ya jeshi la Sudan imeangusha ndege zisizo na rubani za RSF zilizolenga maeneo ya Merowe katika Jimbo la Kaskazini. 

Taarifa ya jeshi la Sudan imesema kwamba ndege hizo zisizo na rubani zilijaribu kulenga Bwawa la Merowe, makao makuu ya Kitengo cha 19, na Kituo cha Anga cha Merowe.

Kitengo cha 19 cha jeshi kimesema kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba kimekabiliana na ndege zisizo na rubani za kujitoa mhanga na kuzitungua kabla hazijatimiza malengo yao, kikithibitisha kwamba hakukuwa na hasara za nafsi au uharibifu wa mali.

Jana Jumapili pia Shirika la Habari la Ufaransa lilinukuu vyanzo vya matibabu vikisema kwamba watu 114 waliuawa katika wiki moja katika mashambulizi tofauti eneo la Darfur magharibi mwa Sudan, huku mapigano yakiongezeka kati ya jeshi la taifa la Sudan na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF).

Chanzo cha matibabu katika Hospitali ya Al-Zarq katika Jimbo la Darfur Kaskazini kimesema kwamba raia 51 waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani siku ya Jumamosi.

Haya yanajiri huku pande mbili zikituhumiana kuhusika na mauaji ya makumi ya watu na kujeruhiwa wengine wengi kutokana na mashambulizi yanayolenga majengo ya raia katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *