Kufuatia shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela na kukamatwa kwa rais wa nchi hiyo, viongozi mbalimbali wa dunia na serikali walionyesha wasiwasi kuhusu matokeo ya hatua hii na kutoa wito wa suluhu ya kidiplomasia ya mgogoro huo, kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa, na kurejea kwenye michakato ya kidemokrasia.
Uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Venezuela na kukamatwa Rais Nicolas Maduro na kisha kupelekwa Marekani umesababisha wimbi la radiamali na mijibizo ya kimataifa. Nchi nyingi zimekitaja kitendo hiki kuwa cha kimabavu na kinyume na kanuni na sheria za kimataifa, na zimeonya kuhusu athari zake kwa utulivu wa kikanda na utaratibu wa kimataifa.
Anwar Ibrahim Waziri Mkuu wa Malaysia ametoa mwito wa kuachiliwa huru mara moja Nicolas Maduro na mkewe, akielezea kukamatwa kwao kama “ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.” Anwar Ibrahim alisisitiza kwamba mustakabali wa kisiasa wa Venezuela unapaswa kuamuliwa tu na watu wa nchi hiyo na kwamba matumizi ya nguvu yanadhoofisha mfumo wa kisheria unaotawala mahusiano ya mataifa ya dunia.
Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya India imesema katika taarifa yake kwamba, matukio ya hivi karibuni “yanatia wasiwasi sana” na kuzitaka pande zote kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo na njia za amani. New Delhi pia ilisisitiza udharura wa kuweko hakikisho la usalama na ustawi wa watu wa Venezuela.
Australia pia ilitoa wito wa kujizuia na kuelezea uungaji mkono wake kwa diplomasia na kukabidhiwa madaraka kwa amani na kidemokrasia. Waziri Mkuu wa nchi hiyo alisisitiza kwamba utulivu katika Ulimwengu wa Magharibi unaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo na kuheshimu sheria za kimataifa.
Japan, Korea Kusini, Ufilipino, na Thailand pia zilitoa taarifa tofauti zikisisitiza haja ya kupunguza mivutano, kurejesha demokrasia, na kuheshimu matakwa ya watu wa Venezuela, huku zikitangaza kupitishwa kwa hatua muhimu za kulinda usalama wa raia wao.

Rais Gustavo Petro wa Colombia ametahadharisha kuwa nchi za Amerika ya Latini ni lazima ziungane, kinyume chake zitakabiliwa na hatari ya kufanywa kama watumwa. Rais wa Colombia ametamka haya kufuatia vitisho mtawalia vya Rais Donald Trump wa Marekani vinavyojumuisha uwezekano wa kufanyika oparesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Jumamosi ilisisitiza katika taarifa yake kwamba: Inalaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.
Russia kwa upande wake imepinga na kulaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kuyataja kuwa haramu na kinyume cha sheria. Konstantin Kosachev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa Telegram akisema kwamba: Venezuela haikuwa tishio kwa Marekani, na kwamba sheria za kimataifa ndizo zinazopaswa kufuatwa, na si sheria za kujibunia”.
Rais Miguel Diaz- Canel wa Cuba ameyataja mashambulizi ya Marekani dhidi ya Caracas kuwa kitendo cha jinai na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.
Serikali ya Uhispania kwa upande wake imesema kuwa iko tayari kusaidia jitihada za kupunguza mivutano na imetaka kuheshimiwa sheria za kimataifa. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania imesisitiza kuwa ipo haja ya kuzuia machafuko zaidi na kwamba ipo tayari kuwa mpatanishi ili kufanikisha mazungumzo na ufumbuzi wa amani.
Naye Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia amesema amekuwa akifuatilai kwa karibu hali ya mambo ya Venezuela akijikita hasa katika kukusanya taarifa kuhusu raia wa Italia wanaoishi Venezuela. Amesema, kwa wastani Wataliano 160,000 wanaoishi Venezuela aghalabu yao wana uraia wa nchi mbili.
Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva amesema: Kushambulia ardhi ya Venezuela na kumkamata rais wake kunavuka mstari usiokubalika na kwamba kitendo hicho ni dharau kubwa kwa mamlakka ya kujitawala Venezuela na mfano hatari sana kwa jamii ya kimataifa.
Barani Afrika pia, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeitaka jamii ya kimataifa kuheshimu uhuru na mamlaka ya kitaifa ya Venezuela kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo yaliyopelekea kukamatwa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe.

Huku ikitambua haki ya nchi mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na ugaidi na biashara haramu ya dawa za kulevya, Jumuiya ya ECOWAS imesema kuwa inapenda kuikumbusha jamii ya kimataifa wajibu wake wa kuheshimu uhuru na mamlaka ya kitaifa ya kila nchi kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hasa kifungu cha 2 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Afrika Kusini imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela, na kukamatwa Rais wa nchi hiyo Nicholas Maduro na mkewe.
Kwa ujumla, radiamali za kimataifa zinaonyesha kwamba, sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa inaamini kwamba, suluhisho la mgogoro wa Venezuela haliko katika hatua za kijeshi, bali katika diplomasia, mazungumzo, na kurudi kwenye mifumo ya kidemokrasia.