Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Shomari Bane, ametangaza nafasi za ajira kwa walimu watakaofundisha katika shule za Serikali za English Medium zinazoanzishwa na Halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha elimu na kuongeza ufaulu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Bane amesema Halmashauri imeanzisha jumla ya shule tatu (3) zenye mchepuo wa Kingereza kuanzia Elimu ya Awali na Msingi, ambazo zinalenga kutoa elimu bora kwa kutumia lugha ya Kingereza.
Amesema lengo la kuanzisha shule hizo za Serikali za English Medium ni kupandisha kiwango cha ufaulu, kuboresha ubora wa elimu pamoja na kuongeza wigo wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kuhusu ajira za walimu, Afisa Elimu huyo amesema Halmashauri inahitaji walimu wenye umahiri wa kufundisha kwa lugha ya Kingereza, ambapo watakaochaguliwa watapitia usaili na mitihani kulingana na somo husika.
Ameongeza kuwa walimu hao wataajiriwa kwa mkataba wa majaribio wa miezi mitatu (3), ili kupima uwezo wao wa kufundisha kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Bane amesema mtihani wa usaili utafanyika Januari 10, 2026, na vigezo vinavyotakiwa kwa waombaji ni kuwa na Elimu ya Stashahada (Diploma), Shahada (Degree) au Uzamili (Master) kulingana na somo wanaloomba kufundisha.
Kwa sasa, Halmashauri ya Jiji la Tanga ina shule tatu za Serikali za English Medium, hatua inayochukuliwa kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha sekta ya elimu katika jiji hilo.