Hifadhi ya Taifa ya Virunga imetangaza kwamba Sokwe wa milimani anayeitwa Mafuko amezaa mapacha wawili wa kiume katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo ambalo limekuwa likikumbwa na vita kwa muda mrefu.

Tukio hili limeelezwa kama hatua muhimu sana katika juhudi za uhifadhi wa aina hii adimu ya sokwe.

Mapacha hao wawili wa kiume walizaliwa na Sokwe Mafuko, na waligunduliwa tarehe Januari 3, 2026 na kulingana na taarifa ya hifadhi hiyo, mapacha hao walionekana kuwa na afya nzuri wakati walipoonekana kwa mara ya kwanza.

Virunga, iliyo na zaidi ya maili za mraba 3,000, ni hifadhi kongwe zaidi barani Afrika na ni makazi ya Sokwe wa milimani waliobaki duniani.

Hata hivyo, maeneo mengi ya hifadhi hiyo yako chini ya udhibiti wa waasi, hali inayosababisha kuongezeka kwa uharibifu wa misitu ya Virunga.

Kulingana na hifadhi ya Virunga, suala la kuwahudumia mapacha huwa na changamoto, hasa katika miezi ya mwanzo ambapo watoto hao wa Sokwe hutegemea kikamilifu  ungalizi kutoka kwa mama. Kwa sasa, wafanyakazi wa hifadhi wanawafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha wanaendelea vyema.

Picha zilizotolewa na hifadhi zinaonyesha mama wa mapacha hao, Mafuko, mwenye umri wa miaka 22, akiwa amewakumbatia watoto wake mapacha, akiwa ameketi chini miongoni mwa matawi yenye majani ya kijani.

Mafuko alizaliwa katika familia ya Kabirizi, lakini alijiunga na familia ya Bageni miaka sita baada ya mama yake kuuawa mwaka 2007 na watu wenye silaha, kulingana na maelezo ya hifadhi ya Virunga.

Hadi sasa Mafuko amezaa Sokwe saba, ikiwemo mapacha waliokufa wiki moja tu baada ya kuzaliwa mwaka 2016. Familia ya Bageni sasa ina jamaa 59, na ndiyo familia kubwa zaidi ya sokwe katika hifadhi hio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *