Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesisitiza kwamba operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela imedhoofisha kanuni na misingi ya sheria ya kimataifa kuhusu kutotumia nguvu. Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Türk ameandika: “Nchi hazipaswi kutumia mabavu kwa ajili ya madai ya kumiliki ardhi au kwa ajili ya kutekeleza matakwa yao ya kisiasa.”
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza kwamba jamii ya Venezuela inahitaji kupata ahueni, akisema: “Mustakabali wa nchi hiyo lazima uamuliwe na watu wake.”

Baada ya miezi kadhaa ya mvutano na Venezuela, alfajiri ya Jumamosi Januari 3, 2026 Marekani ilifanya mashambulizi makubwa ya kijeshi nchini humo, na kumteka nyara Rais Nicolas Maduro na mkewe na kuwahamishia Marekani. Maduro na mkewe walifika kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Shirikisho huko Manhattan, New York, mnamo Januari 5, 2024, kujibu mashtaka yaliyowasilishwa na utawala wa Trump, lakini wamekanusha mashtaka yote dhidi yao. Kesi ya Maduro na mkewe imepangwa kufanyika tena Machi 17.
Hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela imekabiliwa na wimbi la upinzani wa kimataifa, na nchi nyingi zimesisitiza haja ya kuheshimiwa kanuni za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Wawakilishi wa nchi mbalimbali wamekosoa shambulio la kijeshi la utawala wa Trump dhidi ya Venezuela katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na wanachama wengi wa baraza hilo wamelitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 2 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kwamba kutekwa nyara Rais Nicolas Maduro ni ukiukaji usio wa kawaida wa kinga ya wakuu wa nchi na tishio kubwa kwa amani wa nidhamu ya kimataifa. Wameonya dhidi ya kuhalalisha “hatua yoyote ya kubadilisha utawala wa nchi kwa kutumia mabavu” na kusisitiza kwamba hata wasiwasi kuhusu haki za binadamu, demokrasia au uhalifu wa kupangwa si msingi wa kisheria wa hatua za kijeshi zinazovuka mipaka.
Jambo muhimu ni kwamba, Marekani haikupata uungwaji mkono katika Baraza la Usalama, hasa miongoni mwa nchi za Amerika Kusini, na hoja za mwakilishi wake zilikuwa za kisiasa na zililenga kuhalalisha shambulio hilo, jambo ambalo limekabiliwa na upinzani mkubwa wa kimataifa. Swali muhimu ni kwamba, kwa nini Umoja wa Mataifa umetathmini hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela kuwa ni tishio kubwa kwa sheria za kimataifa?
Inaonekana kwamba Umoja wa Mataifa umechukua msimamo huu kwa sababu hatua hiyo inakiuka kanuni za msingi za mfumo wa kimataifa na ina taathira mbaya sana kwa sheria za kimataifa.
Kanuni ya kwanza iliyokiukwa ni ile inayokataza utumiaji wa nguvu na mabavu, ambayo imeelezwa waziwazi katika Kifungu cha 2 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Kifungu hiki kinakataza utumiaji wa mabavu dhidi ya ardhi au mamkala ya kisiasa ya nchi yoyote mwanachama wa UN, isipokuwa katika hali ya kujilinda au kwa idhini ya Baraza la Usalama. Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela yaliyofanyika bila idhini hiyo yanatambuliwa kuwa ni ukiukaji wa wazi wa kanuni hii, na kwa sababu hiyo Umoja wa Mataifa unasema kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Kanuni ya pili iliyokiukwa na Marekani ni ile ya ulazima wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa wa nchi wanachama. Sheria za kimataifa zinategemea kanuni hiyo, na uingiliaji wowote katika mambo ya ndani ya nchi nyingine ni kinyume chake. Uvamizi wa vikosi vya jeshi la Marekani katika ardhi ya Venezuela na kumteka nyara rais wa nchi hiyo ni ukiukaji wa moja kwa moja wa mamlaka ya taifa ya nchi huru. Kitendo hiki kinaonyesha kwamba dola kubwa linaweza kulazimisha matakwa yake kwa nchi nyingine bila kuzingatia sheria za kimataifa, na hili linadhoofisha imani ya watu kwa mfumo wa kisheria wa kimataifa.

Umoja wa Mataifa pia unasisitiza kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Kubadilisha uongozi wa kisiasa wa nchi kupitia hatua za kijeshi za dola la kigeni ni mfano wa wazi wa uingiliaji kati kinyume cha sheria. Kitendo kama hicho hakivunji tu nidhamu ya ndani ya nchi inayolengwa, lakini pia hujenga muundo hatari kwa mataifa mengine yenye nguvu na kutayarisha mazingira ya ukosefu wa utulivu katika mahusiano ya kimataifa.
Kwa upande mwingine, mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela yamefanyika bila idhini ya Baraza la Usalama, ambalo ndilo mamlaka pekee halali ya kuidhinisha matumizi ya nguvu katika ngazi ya kimataifa. Kupuuza taasisi hiyo kunadhoofisha hadhi yake na kuibua shaka kuhusu nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na usalama duniani. Iwapo vitendo hivyo vya upande mmoja vitarudiwa, Baraza la Usalama halitakuwa na ufanisi wowote, na maamuzi ya mtu binafsi kutoka kwa mataifa makubwa yatachukua nafasi ya mfumo wa pamoja wa kimataifa.
Kwa ujumla ni kwamba, Umoja wa Mataifa umeitambua hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela kuwa si tukio la kijeshi tu, bali pia tishio kwa sheria za kimataifa.