Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel amefanya safari huko Hargeisa, mji mkuu wa eneo la Somaliland, akiongoza ujumbe rasmi wa Israel.
Gideon Saar alipangiwa kukutana na Abdulrahman Mohammed Abdullah, rais aliyejitangaza mwenyewe wa eneo hilo lililojitenga na Somalia, kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupanua ushirikiano wa kidiplomasia, usalama na kiuchumi; hatua ambayo inaonekana kama mwendelezo wa sera za kujitanua na uvamizi za Tel Aviv barani Afrika.
Safari hii inakuja yapata siku kumi baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuitambua rasmi Somaliland kama nchi huru katika hatua haramu na ya kichokozi dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya nchi ya Somalia, hatua ambayo imeibua hasira kubwa katika jamii ya kimataifa.
Safari ya Gideon Saar huko Somaliland inapaswa kutambuliwa kuwa ni zaidi ya ziara ya kawaida ya kidiplomasia. Tukio hilo ni ishara ya wazi ya kuingia rasmi Israel katika milinganyo ya kijiopolitiki ya Pembe ya Afrika, eneo ambalo limekuwa kitovu cha ushindani kati ya madola ya kikanda na nje ya kanda hiyo kutokana na kuwa jirani wa Bahari Nyekundu, mlango bahari wa Bab el-Mandeb na njia muhimu za usafirishaji wa nishati na biashara ya kimataifa.
Ushawishi wa utawala wa Kizayuni barani Afrika ni matokeo ya mkakati wa muda mrefu na wa taratibu ulioanza miongo kadhaa iliyopita. Israel, ambayo imeshindwa kuvutia uungaji mkono na ushirikiano wa nchi za eneo la Asia Magharibi kwa miongo kadhaa, inajaribu kupunguza kutengwa kwake kisiasa kwa kugeukia Afrika. Kwa hivyo, imeweza kupenya na kuwa na ushawishi katika baadhi ya nchi za Afrika kwa kutumia mitego kama vile ushirikiano katika masuala ya usalama, mafunzo ya kijeshi, teknolojia za ufuatiliaji, kilimo cha kisasa na misaada ya kiufundi. Ushawishi huu umefanikiwa katika nchi ambazo zinakabiliwa na migogoro ya ndani, migawanyiko ya kikabila, au miundo dhaifu ya serikali, ikiwa ni pamoja na Somalia.
Katika ngazi ya kisiasa, utawala wa Kizayuni wa Israel pia umejaribu kuunda mtandao wa washirika wadogo lakini waaminifu kwa kuunga mkono harakati za kisiasa zinazoibuka au harakati za kujitenga. Wachambuzi wengi pia wanatathmini nafasi ya Israel katika matukio ya Sudan Kusini katika muktadha huu, mtindo ambao sasa unakaririwa huko Somaliland. Lengo kuu la mbinu hii ni kuunda mazingira yanayokidhi maslahi haramu ya Israel.
Katika suala la usalama, Afrika imekuwa maabara ya Israel kupanua na kuuza nje teknolojia za habari na ufuatiliaji. Uwepo Israel huko Somaliland utairuhusu Tel Aviv kupeleka mifumo yake ya udukuzi, ufuatiliaji wa kielektroniki na kufuatilia harakati na safari za baharini katika mojawapo ya maeneo nyeti zaidi duniani, bila kulipa gharama za kisiasa za kupeleka maafisa wake katika nchi kubwa na zinazojulikana.
Swali muhimu hapa ni kwamba, ni nini lengo mahususi la Israel la kutambua rasmi eneo la Somaliland huko Somalia kama nchi huru? Lengo la kwanza na la msingi zaidi la kimkakati la utawala wa Kizayuni katika Pembe ya Afrika ni udhibiti na usimamizi usio wa moja kwa moja juu ya mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya kijiografia duniani, yaani lango bahari la Bab el-Mandeb na njia yake ya kuelekea Bahari Nyekundu. Lango hilo ni njia kubwa ya biashara ya kimataifa, nishati na usafirishaji wa bidhaa kati ya Asia, Ulaya na Afrika. Kuwepo zana za ujasusi za Israel huko Somaliland kutaiwezesha Tel Aviv sio tu kufuatilia harakati za baharini za washindani na wapinzani, lakini pia kunaipa wenzo bora wa shinikizo kwenye njia za meli.
Lengo la pili ni kudhibiti na kuuzingira kimkakati Mhimili wa Muqawama katika ngazi ya kikanda. Tel Aviv inaiona Somaliland kama kiungo kinachokamilisha mnyororo wa kuanzia mashariki mwa Mediterania hadi Bahari Nyekundu na Pembe ya Afrika. Uwepo wa Israel katika eneo hilo utauruhusu utawala wa Kizayuni kufuatilia matukio ya Yemen na harakati za Ansarullah katika maji ya kusini. Kwa mtazamo huu, Somaliland si mshirika wa kisiasa tu, bali ni jukwaa la operesheni ya kukamilisha ukanda wa usalama wa Israel kuzunguka Rasi ya Arabia na Afrika Mashariki.
Lengo la tatu ni kuunda na kuimarisha wachezaji tegemezi wa kisiasa katika maeneo yenye misukosuko. Tel Aviv inaelewa vyema kwamba serikali kuu dhaifu au maeneo yanayotaka kujitenga yako tayari zaidi kuliko mengine kukubali himaya ya kiusalama na msaada wa kisiasa wa kigeni. Kutokana na kutotambuliwa rasmi kimataifa, Somaliland inahitaji sana himaya ya madola yenye nguvu, na hii ndiyo nukta inayotumiwa vibaya na Tel Aviv.
Lengo la nne la kimkakati ni kuarifisha upya nafasi ya Israel katika siasa za Afrika. Kwa kuwepo kikamilifu katika eneo la Pembe ya Afrika, Tel Aviv inajaribu kuonyesha kwamba ina uwezo wa kuwa na nafasi muhimu katika matukio ya bara hilo.
Lengo lingine la utawala wa Kizayuni ni kutumia Somaliland kama mahali pa kuwahamishia Wapalestina wanaofukuzwa Ukanda wa Gaza; mpango ambao umependekezwa katika duru za kisiasa za Israel na unaonyesha njama za utawala huo za kubadilisha muundo wa idadi ya watu huko Palestina.

Ingawa utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya juhudi za kuendeleza sera zake bila kujali malalamiko ya jamii ya kimataifa, lakini upinzani dhidi ya hatua hiyo bado unaendelea, hata kutoka kwa baadhi ya washirika wa Tel Aviv. Msimamo huu si kwamba unatokana na tofauti za kisiasa, bali kwa sababu ya wasiwasi mkubwa wa kiusalama, kisheria na kihistoria.
Serikali kuu ya Somalia inakiona kitendo hicho kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka yake ya kitaifa na ina wasiwasi kwamba kutambua rasmi Somaliland kutasababisha wimbi jipya la kutaka kujitenga nchini humo na hata kote katika Pembe ya Afrika. Nchi nyingi za Kiafrika, kutokana na uzoefu mchungu wa kipindi cha ukoloni, pia zimeonya dhidi ya uungaji mkono wowote wa kigeni kwa harakati za kujitenga.
Katika ngazi ya kikanda, nchi za Kiarabu na Kiislamu zinahofia kwamba uwepo wa Israel katika Pembe ya Afrika utavuruga mlingano wa kiusalama katika Bahari Nyekundu na kugeuza eneo hilo kuwa uwanja wa makabiliano ya moja kwa moja na ya gharama kubwa.
Mwishoni inatupasa kusema kuwa, kinachoendelea nyuma ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel huko Somaliland si mpango halali wa kidiplomasia, bali ni jaribio lililoshindwa la kutumia kwa muda migogoro na mapengo ya kimuundo katika nchi za Afrika.