
Katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: Washington lazima imzuie Netanyahu kuvuruga juhudi za maelewano kwa sababu hakuna amani wala utulivu wowote utakaopatikana Lebanon na katika eneo zima la Asia Magharibi bila kukomeshwa uvamizi na ukaliaji mabavu wa ardhi za nchi za eneo.
Saeed Khatibzadeh, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran iko tayari kuendelea na mazungumzo hatua kwa hatua iwapo upande wa pili utaonyesha nia nzuri, na kusisitiza kuwa, makubaliano yoyote yanayowezekana katika siku za usoni lazima yajumuishe kuachiliwa kwa mali zote zinazozuiliwa na rasilimali za kifedha za Iran.
Akigusia mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel huko Lebanon, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Washington lazima itekeleze hati ya maelewano na kumzuia Netanyahu kwa njia yoyote ile, kukwamisha juhudi za maelewano na kupatikana uthabiti katika eneo.
Khatibzadeh ameiambia Al Jazeera: “Tunajaribu kufikia amani katika pande zote, ikiwa ni pamoja na Gaza, na tumeijumuisha Lebanon katika mkataba huu wa maelewano kwa sababu ya kuathirika kwake moja kwa moja na vita. Bila ya kukomesha uvamizi huo na bila ya Israel kufuata sheria za kimataifa, hakutakuwa na amani wala utulivu huko Lebanon na katika eneo zima.”
Akijibu tuhuma na madai yasiyo na msingi yanayotolewa na pande hasimu dhidi ya Iran amesema: “Hatutaki kutawala eneo hili na tuna maslahi ya pamoja na nchi zote za eneo.”
Kuhusu suala la Lango-Bahari la Hormuz, pia amesema: “Tutatoa huduma za meli katika lango la Hormuz kwa ushirikiano na Usultani wa Oman na kwa mujibu wa sheria za kimataifa; tuna haki za kisheria katika Lango-Bahari la Hormuz, lakini hatutatoza ada au malipo yoyote katika kipindi cha siku 60, na baada ya siku 60 tutakeleza mchakato mpya wa Hormuz, na kuanzisha ubunifu maalum kwa ajili ya nchi za eneo.”