Wanaume 127 kati ya165 Mkoani Dar es saalaam wamegundulika na ugonjwa wa mabusha baada ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa ugonjwa huo ambapo watu 27 wamefanyiwa upasuaji bila malipo tangu kuanza kwa kampeni ya upasuaji wa ugonjwa huo Januari 5 mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule akitoa taarifa kuhusu kambi ya upasuaji wa Mabusha mkoani Dar es salaam, amesema kambi hiyo itaendeshwa kwa siku 25 kuanzia Januari 5 hadi 30 huku akiwataka wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi na upasuaji bila malipo kwa watakaobainika kuwa na ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Mohamed Mang’una, amesema kambi za uchunguzi wa awali katika kampeni ya upasuaji wa mabusha zipo kwenye hospitali zote za wilaya mkoani humo wakati upasuaji unafanyika katika vituo viwili pekee kituo cha afya Kinondoni na kituo cha afya Kilakala kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Meneja Mpango wa Taifa Udhibiti Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya Dkt. Clara Mwansasu, amebainisha kuwa kwenye kata 10 za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni bado maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha yapo juu.

Kampeni ya upasuaji wa mabusha bila malipo kwa mkoa wa Dar es salaam inatarajiwa kuwafikia wakazi 500 wenye ugonjwa wa mabusha katika siku 25 ambapo Waziri wa afya anafanya uzinduzi rasmi Januari 20 mwaka huu.

#StarTvaupdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *