Mkataba wa Mercosur unapigiwa debe na makundi ya kibiashara lakini unapingwa na wakulima wengi wa Ulaya.
Kwenye mkutano wa wawakilishi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji, idadi kubwa ya washiriki waliridhia kusainiwa kwa mkataba huo. Hayo ni kulingana na wanadiplomasia.
Mkataba mpya wa Mercosur utakaoruhusu biashara kwa zaidi ya watu milioni 700, wa nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani Kusini ikiwemo Brazil, Argentina, Uruguay na Paraguay, ndio utakuwa mkataba mkubwa zaidi wa aina yake duniani kote. Kamisheni kuu ya Umoja wa Ulaya imedokeza.
Kitakachofuata sasa ni kwamba huenda rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akatia sainimkataba huo wiki ijayo pamoja na washirika wao wa kusini mwa Amerika.
Ujerumani, Uhispania na nchi nyingine zinazounga mkono mkataba huo, zinaamini utapiga jeki viwanda vyao vinavyotatizwa na ushindani mkali kutoka China na vilevile athari za ushuru kutoka Marekani na China.
Ujerumani yaunga mkono mkataba wa kibiashara wa Mercosur
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alikaribisha uungwaji mkono wa mkataba huo akisema ni hatua muhimu katika sera ya kibiashara ya Ulaya na inaashiria uhuru wao wa kimkakati na uhuru wa kuchukua hatua.
Makubaliano kuhusu mkataba huo wenye utata yalifanikishwa baada ya serikali kutoa msamaha zaidi kwa kundi la wakulima.
Kundi hilo linahofia ushindani kutoka nchi nne wanachama wa muungano mpana wa kibiashara wa Mercosur barani Amerika Kusini kama tishio kwa wakulima wa Ulaya.
Huko Kusini mwa Amerika, bidhaa za kilimo kama nyama zinaweza kuzalishwa kwa njia nafuu kuliko Ulaya.
Ridhaa ya Italia yaipa Mercosur uhai
Ridhaa ya Italia ilikuwa muhimu kwa sababu Ufaransa na Poland ambazo ni nchi mbili zenye idadi kubwa ya watu katika Umoja wa Ulaya, tayari zinaupinga mkataba huo jinsi ulivyo kwa sasa. Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia anaeleza: “Mimi naona uwiano uliowekwa utakuwa endelevu, na natumai makubaliano hayo yataleta manufaa katika nyanja nyingi, kama ninavyoamini, na kwa matumaini ya kila mtu.”
Awali, mkataba huo ulipaswa kusainiwa mwezi Disemba nchini Brazil. Lakini idadi iliyohitajika ya nchi za Umoja wa Ulaya kuridhia haikutimia kwa sababu Itali ilisita kwa kusimama na matakwa ya wakulima wa Ulaya.
Lau wangeshindwa kuridhia mkataba huo, basi huenda ingekuwa mwisho wake kabisa, kwa sababu mwezi uliopita Brazil ilitishia kujiondoa iwapo Umoja wa Ulaya ungeendelea kuahirisha maamuzi.
Maandamano ya kupinga Mercosur yazuka Poland, Ufaransa na Italia
Mkataba huo ulihitaji uungwaji mkono wa angalau nchi 15 za Umoja wa Ulayamiongoni mwa jumla ya 27, hiyo ikiwa ni asilimia 65 ya wanachama katika umoja huo.
Ufaransa na wakosoaji wengine waliupinga kufuatia wasiwasi wa wakulima kwamba kuingizwa kwa bidhaa za bei nafuu kutoka kusini mwa Amerika ikiwemo nyama, sukari, asali na mchele, kunaweza kutaathiri mauzo ya bidhaa zao.
Punde baada ya nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuukubali mkataba huo, wakulima waliandamana mjini Warsaw huko Poland kuonyesha kutoridhishwa kwao. Maandamano kama hayo pia yameshuhudiwa Ufaransa na Italia.
DPAE; AFPE