Aliyempa Zidane jina ‘Zizou’ afariki dunia akiwa na miaka 72Aliyempa Zidane jina ‘Zizou’ afariki dunia akiwa na miaka 72

Mchezaji wa zamani wa soka wa Ufaransa, kocha na mchambuzi wa michezo kwenye vyombo vya habari, Rolland Courbis amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72.

Nyota huyo wa zamani aliyempatia jina la Zizou nyota wa zamani wa soka Zinedine Zidane amefariki usiku wa kuamkia Jumatatu Januari 12, 2026 nchini Ufaransa, huku sababu za kifo chake hazijawekwa wazi.

Kazi yake ya ukocha pia ilimfikisha Bordeaux, Lens, Montpellier na USM Alger. Akiwa Bordeaux, alimfundisha Zidane na inaelezwa kuwa yeye ndiye aliyempa jina la utani lililodumu la Zizou.

Zidane amwelezea kocha wake huyo wa zamani akisema namna alivyokuwa na mchango katika maisha yake ya soka.

“Alimaanisha mengi sana kwangu kama kocha na pia kibinafsi; alikuwa mtu wa kupendeka sana na wa kweli,” Zidane aliandika kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu.

Courbis aliyezaliwa mjini Marseille, alikulia katika akademi ya klabu hiyo ya Marseille na akaingia kikosi cha kwanza kama beki.

Alikuwa sehemu ya timu iliyotwaa ubingwa wa ligi ya Ufaransa na Kombe la Ufaransa mwaka 1972 na alirejea klabuni humo mwishoni mwa miaka ya 1990 akiwa kocha.

Akiwa mchezaji, pia alishinda mataji mawili ya ligi ya Ufaransa na Kombe la Ufaransa akiwa na Monaco.

“Kwa moyo na roho alikuwa Mmarseille. Aliwakilisha soka la watu wa kawaida, lenye nguvu na uhai. Lafudhi yake ya kipekee ilibeba maneno yake ya wazi, ya moja kwa moja, mara nyingi yenye shauku na daima ya dhati,” imeandika klabu ya Marseille katika salamu zake za rambirambi.

Miongoni mwa matukio yaliyobaki kukumbukwa katika taaluma ya Courbis ni kurejea kwa kushangaza alikosimamia akiwa kocha wa Marseille. Timu yake ilikuwa nyuma kwa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Montpellier mwaka 1998, lakini ilipambana na hatimaye kushinda kwa mabao 5-4.

Maisha yenye misukosuko

Courbis aliwahi kuishi kwa muda na kiongozi wa kifalme kutoka Italia (countess), na aliishi maisha yenye misukosuko. Mwaka 1996, alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati watu wenye silaha walipomuua rais wa klabu moja ya Ufaransa nje ya uwanja. Courbis pia aliwahi kuhusika katika kesi za kisheria na kuhukumiwa kifungo cha gerezani.

Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amesema kuwa kwa kifo cha Courbis, soka la Ufaransa limepoteza “mtaalamu wa soka na mifumo yake ya ndani, pamoja na mchezo wenyewe.”

Baada ya kuacha ukocha mwaka 2002, Courbis alikuwa maarufu katika tasnia ya vyombo vya habari vya michezo akifanya kazi kama mchambuzi wa redioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *