Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi ameionya Marekani kwamba, Tehran “iko tayari kwa machaguo yote” baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuchukua hatua za kijeshi sambamba na Iran kukabiliwa na machafuko hivi karibuni yaliyochochewa na kuungwa mkono na maadui wa nje ya nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na televisheni ya Al Jazeera, Araghchi amesema, njia za mawasiliano na Marekani zimekuwa wazi sambamba na machafuko yaliyotokea nchini, akisisitiza kwamba Tehran iko tayari kwa vita ikiwa Washington inataka “kuvijaribu”.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Iran hivi sasa ina “utayarifu mkubwa na mpana wa kijeshi” ikilinganishwa na wakati wa uchokozi wa kijeshi wa siku 12 uliofanywa kwa ushirikiano wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel mnamo mwezi Juni mwaka jana. Uvamizi huo, ambao ulipelekea kuuawa shahidi zaidi ya Wairani elfu moja, ulifanywa wakati Tehran na Washington zilipokuwa katikati ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana ya kujadili kadhia ya nyuklia ya Iran.

Araghchi ametangaza msimamo huo kufuatia matamshi aliyotoa Trump siku ya Jumapili ambapo alidai kuwa, anafikiria “machaguo makali” ya kuchukua dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuishambulia kijeshi kwa madai ya alichokiita makabiliano ya Jamhuri ya Kiislamu na waandamanaji.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kwamba, ikiwa “Washington inataka kujaribu chaguo la kijeshi ambalo imeshalijaribu hapo kabla, tuko tayari kwa hilo.”

Pamoja na hayo, amesema ana matumaini kuwa, Marekani itachagua “chaguo la busara” la mazungumzo, huku akionya kuhusu “wale wanaojaribu kuiingiza Washington vitani ili kuhudumia maslahi ya Israel.”

Katika mahojiano hayo na Al Jazeera, Araghchi aidha amesema, mawasiliano kati ya yake na Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff “yaliendelea kabla na baada ya maandamano na yangali yanaendelea.”

Amefafanua kuwa, maoni ambayo wameyajadili na Washington yanapitiwa mjini Tehran. Hata hivyo, ameongezea kwa kusema, “maoni yaliyopendekezwa na Washington na vitisho vyake dhidi ya nchi yetu haviendani pamoja.”

“Tuko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia, mradi tu ni bila ya kutolewa vitisho au amri,” ameeleza bayana Araghchi, huku akihoji kama Washington iko “tayari kweli kwa mazungumzo ya usawa na ya haki” na akasisitiza kwa kusema: “itapokuwa tayari, tutazingatia jambo hilo kwa uzito”.

Maandamano ya amani yaliyofanyika wiki iliyopita kulalamikia hali ngumu ya kiuchumi hapa nchini Iran yalipamba moto baada ya kubadilika kuwa ya vurugu na machafuko, yakichochewa na matamshi ya viongozi wa Marekani na Israel, huku makundi ya wabeba silaha yakiharibu mali za umma na kusababisha maafa ya roho za watu miongoni mwa raia wa kawaida na askari wa vikosi vya usalama.

Vyombo vya usalama na vya Idara ya Mahakama vimesema, wakati wa machafuko hayo, vimesambaratisha seli kadhaa za wabeba silaha na kuwakamata washambuliaji wenye mfungamano na madola ya kigeni…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *